Nahumu 1
1 Ufunuo juu ya Ninawi. Kitabu cha maono aliyoyaona Nahumu, Mwelkoshi.
2 Bwana ni Mungu mwenye wivu, naye hujilipiza kisasi; Bwana hujilipiza kisasi, naye ni mwingi wa hasira; Bwana hujilipiza kisasi juu ya adui zake, huwawekea adui zake akiba ya hasira.
3 Bwana si mwepesi wa hasira, ana uweza mwingi, wala hatamhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; Bwana ana njia yake katika kisulisuli na tufani, na mawingu ni mavumbi ya miguu yake.
4 Yeye huikemea bahari na kuikausha, pia huikausha mito yote; Bashani hulegea, na Karmeli; hulegea nalo ua la Lebanoni.
5 Milima hutetema mbele zake, navyo vilima huyeyuka; nayo dunia huinuliwa mbele za uso wake, naam, dunia na wote wakaao ndani yake.
6 Ni nani awezaye kusimama mbele za ghadhabu yake, naye ni nani awezaye kukaa katika ukali wa hasira yake? Hasira yake kali humwagwa kama moto, nayo majabali yapasuliwa na yeye.
7 Bwana ni mwema, ni ngome siku ya taabu; naye huwajua hao wamkimbiliao.
8 Lakini kwa gharika ifurikayo atapakomesha kabisa mahali pake, na kuwafuatia adui zake hata gizani.
9 Mnawaza nini juu ya Bwana? Yeye atakomesha kabisa; mateso hayatainuka mara ya pili.
10 Kwa maana wangawa kama miiba iliyotatana, na kunyweshwa kana kwamba ni katika kunywa kwao, wataliwa kabisa kama mabua makavu.
11 Ametoka mmoja kwako, aniaye mabaya juu ya Bwana, atoaye mashauri yasiyofaa kitu.
12 Bwana asema hivi, Ijapokuwa wana nguvu zilizo timilifu, ijapokuwa ni wengi, hata hivyo watakatwa, naye atapita na kwenda zake. Ingawa nimekutesa, sitakutesa tena.
13 Na sasa nitakuvunjia nira yake, nami nitakupasulia mafungo yako.
14 Tena Bwana ametoa amri katika habari zako, ya kwamba asipandwe tena mtu awaye yote mwenye jina lako; toka nyumba ya miungu yako nitakatilia mbali sanamu ya kuchora, na sanamu ya kuyeyusha; nitakufanyia kaburi lako; kwa maana u mbovu.
15 Tazama, juu ya milima iko miguu yake aletaye habari njema, atangazaye amani. Zishike sikukuu zako, Ee Yuda, uziondoe nadhiri zako; kwa maana yule asiyefaa kitu hatapita kati yako tena kamwe; amekwisha kukatiliwa mbali.