«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Mathayo 16

1  Wakamjia Mafarisayo na Masadukayo, wakamjaribu, wakamwomba awaonyeshe ishara itokayo mbinguni.

2  Akajibu, akawaambia, [Kukiwa jioni, mwasema, Kutakuwa na kianga; kwa maana mbingu ni nyekundu.

3  Na asubuhi, mwasema, Leo kutakuwa na dhoruba; kwa maana mbingu ni nyekundu, tena kumetanda. Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa mbingu; lakini, je! Ishara za zamani hizi hamwezi kuzitambua?]

4  Kizazi kibaya na cha zinaa chataka ishara; wala hakitapewa ishara, isipokuwa ishara ya Yona. Akawaacha, akaenda zake.

5  Nao wanafunzi wakaenda hata ng'ambo, wakasahau kuchukua mikate.

6  Yesu akawaambia, Angalieni, jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.

7  Wakabishana wao kwa wao, wakisema, Ni kwa sababu hatukuchukua mikate.

8  Naye Yesu akafahamu, akawaambia, Mbona mnabishana ninyi kwa ninyi, enyi wa imani chache, kwa sababu hamna mikate?

9  Hamjafahamu bado, wala hamkumbuki ile mikate mitano kwa wale elfu tano, na vikapu vingapi mlivyoviokota?

10  Wala ile mikate saba kwa watu elfu nne, na makanda mangapi mliyoyaokota?

11  Imekuwaje hamkufahamu ya kuwa si kwa sababu ya mkate naliwaambia? Ila jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo.

12  Ndipo walipofahamu ya kuwa hakuwaambia kujilinda na chachu ya mkate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.

13  Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?

14  Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.

15  Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?

16  Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.

17  Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.

18  Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.

19  Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.

20  Ndipo alipowakataza sana wanafunzi wake wasimwambie mtu ye yote ya kwamba yeye ndiye Kristo.

21  Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka.

22  Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata.

23  Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.

24  Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.

25  Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.

26  Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?

27  Kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake; ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.

28  Amin, nawaambieni, Pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika ufalme wake.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23