Marko 15
1 Mara kulipokuwa asubuhi wakuu wa makuhani walifanya shauri pamoja na wazee na waandishi na baraza nzima, wakamfunga Yesu, wakamchukua, wakamleta mbele ya Pilato.
2 Pilato akamwuliza, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu, akamwambia, Wewe wasema.
3 Nao wakuu wa makuhani walikuwa wakimshitaki mambo mengi.
4 Pilato akamwuliza tena akisema, Hujibu neno? Tazama ni mambo mangapi wanayokushitaki!
5 Wala Yesu hakujibu neno tena, hata Pilato akastaajabu.
6 Basi wakati wa sikukuu huwafungulia mfungwa mmoja, wamwombaye.
7 Palikuwa na mtu aitwaye Baraba, amefungwa pamoja na watu waliofanya fitina, na kufanya uuaji katika fitina ile.
8 Makutano wakaja, wakaanza kuomba awafanyie kama vile alivyozoea.
9 Pilato akawajibu, akisema, Je! Mnataka niwafungulie mfalme wa Wayahudi?
10 Kwa maana alitambua ya kuwa wakuu wa makuhani wamemtoa kwa husuda.
11 Lakini wakuu wa makuhani wakawataharakisha makutano, kwamba afadhali awafungulie Baraba.
12 Pilato akajibu tena akawaambia, Basi nimtendeje huyu mnayemnena kuwa ni mfalme wa Wayahudi?
13 Wakapiga kelele tena, Msulibishe.
14 Pilato akawaambia, Kwani, ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, Msulibishe.
15 Pilato akipenda kuwaridhisha makutano, akawafungulia Baraba; akamtoa Yesu, baada ya kumpiga mijeledi, ili asulibiwe.
16 Nao askari wakamchukua ndani ya behewa, ndiyo Praitorio (yaani, nyumba ya uliwali), wakakusanya pamoja kikosi kizima.
17 Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani;
18 wakaanza kumsalimu, Salamu, Mfalme wa Wayahudi!
19 Wakampiga mwanzi wa kichwa, wakamtemea mate, wakapiga magoti, wakamsujudia.
20 Hata wakiisha kumdhihaki, wakamvua lile vazi la rangi ya zambarau, wakamvika mavazi yake mwenyewe; wakamchukua nje ili wamsulibishe.
21 Wakamshurutisha mtu aliyekuwa akipita, akitoka mashamba, Simoni Mkirene, baba yao Iskanda na Rufo, ili auchukue msalaba wake.
22 Wakamleta mpaka mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa.
23 Wakampa mvinyo iliyotiwa manemane, asiipokee.
24 Wakamsulibisha, wakagawa mavazi yake, wakayapigia kura kila mtu atwae nini.
25 Basi ilikuwa saa tatu, nao wakamsulibisha.
26 Palikuwa na anwani ya mashitaka yake iliyoandikwa juu, MFALME WA WAYAHUDI.
27 Na pamoja naye walisulibisha wanyang'anyi wawili, mmoja mkono wake wa kuume na mmoja mkono wake wa kushoto. [
28 Basi andiko likatimizwa linenalo, Alihesabiwa pamoja na waasi.]
29 Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisa-tikisa vichwa, wakisema, Ahaa! Wewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga katika siku tatu,
30 jiponye nafsi yako, ushuke msalabani.
31 Kadhalika na wakuu wa makuhani wakamdhihaki wao kwa wao, pamoja na waandishi, wakisema, Aliponya wengine; hawezi kujiponya mwenyewe.
32 Kristo, mfalme wa Israeli, na ashuke sasa msalabani tupate kuona na kuamini. Hata wale waliosulibiwa pamoja naye wakamfyolea.
33 Na ilipokuwa saa sita, palikuwa na giza juu ya nchi yote, hata saa tisa.
34 Na saa tisa Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?
35 Na baadhi yao waliosimama pale, walisema, Tazama, anamwita Eliya.
36 Na mmoja akaenda mbio, akajaza sifongo siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha, akisema, Acheni, na tuone kwamba Eliya anakuja kumtelemsha.
37 Naye Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho.
38 Pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini.
39 Basi yule akida, aliyesimama hapo akimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema, Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu.
40 Palikuwako na wanawake wakitazama kwa mbali; miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo mdogo na Yose, na Salome;
41 hao ndio waliofuatana naye huko Galilaya, na kumtumikia; na wengine wengi waliopanda pamoja naye mpaka Yerusalemu.
42 Hata ikiisha kuwa jioni, kwa sababu ni Maandalio, ndiyo siku iliyo kabla ya sabato,
43 akaenda Yusufu, mtu wa Arimathaya, mstahiki, mtu wa baraza ya mashauri, naye mwenyewe anautazamia ufalme wa Mungu; akafanya ujasiri, akaingia mbele ya Pilato akauomba mwili wake Yesu.
44 Lakini Pilato akastaajabu, kwamba amekwisha kufa. Akamwita yule akida, akamwuliza kwamba amekufa kitambo.
45 Hata alipokwisha kupata hakika kwa yule akida, alimpa Yusufu yule maiti.
46 Naye akanunua sanda ya kitani, akamtelemsha, akamfungia ile sanda, akamweka katika kaburi lililochongwa mwambani; akavingirisha jiwe mbele ya mlango wa kaburi.
47 Nao Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yose wakapatazama mahali alipowekwa.