«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Marko 12

1  Akaanza kusema nao kwa mifano; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akazungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri.

2  Hata kwa wakati wake akatuma mtumwa kwa wale wakulima, ili apokee kwa wakulima katika matunda ya mizabibu.

3  Wakamtwaa, wakampiga, wakamtoa nje, hana kitu.

4  Akatuma tena kwao mtumwa mwingine, na huyo wakamtia jeraha za kichwa, wakamfanyia jeuri.

5  Akamtuma mwingine, huyo wakamwua; na wengine wengi, hawa wakiwapiga na hawa wakiwaua.

6  Basi alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye akamtuma kwao mwisho, akisema, Watamstahi mwanangu.

7  Lakini wale wakulima wakasemezana, Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu.

8  Wakamkamata, wakamwua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu.

9  basi atafanyaje yule bwana wa shamba la mizabibu? Atakuja na kuwaangamiza wale wakulima, na lile shamba la mizabibu atawapa wengine.

10  Hata andiko hili hamjalisoma, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni.

11  Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu?

12  Nao wakatafuta kumkamata, wakaogopa mkutano; maana walitambua ya kwamba ule mfano amewanenea wao. Wakamwacha wakaenda zao.

13  Wakatuma kwake baadhi ya Mafarisayo na Maherodi, ili wamnase kwa maneno.

14  Hata walipofika walimwambia, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, wala hujali cheo cha mtu; kwa maana hutazami sura za watu; lakini katika kweli waifundisha njia ya Mungu. Je! Ni halali kumpa Kaisari kodi au siyo?

15  Tumpe, tusimpe? Naye, akijua unafiki wao, akawaambia, Mbona mmenijaribu? Nileteeni dinari niione.

16  Wakaileta. Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii na anwani hii? Wakamwambia, Ni ya Kaisari.

17  Yesu akajibu, akawaambia, Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na yaliyo ya Mungu mpeni Mungu. Wakamstaajabia sana.

18  Kisha Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza na kusema,

19  Mwalimu, Musa alituandikia ya kwamba ndugu ya mtu akifa, akamwacha mkewe wala hana mtoto, ndugu yake amtwae yule mkewe akampatie ndugu yake mzao.

20  Basi kulikuwa na ndugu saba, wa kwanza akatwaa mke, akafa, asiache mzao.

21  Wa pili naye akamtwaa akafa, wala yeye hakuacha mzao. Na wa tatu kadhalika;

22  hata na wote saba, wasiache mzao. Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye.

23  Basi, katika kiyama atakuwa mke wa yupi katika hao? Maana wote saba walikuwa naye.

24  Yesu akajibu, akawaambia, Je! Hampotei kwa sababu hii, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu?

25  Kwa maana watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika walioko mbinguni.

26  Na kwa habari ya wafu ya kwamba wafufuliwa, hamjasoma katika kitabu cha Musa, Sura ya Kijiti, jinsi Mungu alivyomwambia, akisema, Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo?

27  Yeye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai. Hivyo mwapotea sana.

28  Na mmojawapo wa waandishi akafika, akawasikia wakisemezana naye, akatambua ya kuwa amewajibu vema, akamwuliza, Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?

29  Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja;

30  nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote.

31  Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.

32  Yule mwandishi akamwambia, Hakika, Mwalimu, umesema vema ya kwamba Mungu ni mmoja, wala hakuna mwingine ila yeye;

33  na kumpenda yeye kwa moyo wote, na kwa ufahamu wote, na kwa nguvu zote, na kumpenda jirani kama nafsi yako, kwafaa kuliko sadaka nzima za kuteketezwa na dhahibu zote pia.

34  Naye Yesu, alipoona kwamba amejibu kwa busara, alimwambia, Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu. Wala hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea hapo.

35  Hata Yesu alipokuwa akifundisha katika hekalu, alijibu, akasema, Husemaje waandishi ya kwamba Kristo ni Mwana wa Daudi?

36  Daudi mwenyewe alisema, kwa uweza wa Roho Mtakatifu, Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwawekapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako.

37  Daudi mwenyewe asema ni Bwana; basi amekuwaje mwanawe? Na mkutano mkubwa walikuwa wakimsikiliza kwa furaha.

38  Akawaambia katika mafundisho yake, Jihadharini na waandishi, wapendao kutembea wamevaa mavazi marefu, na kusalimiwa masokoni,

39  na kuketi mbele katika masinagogi, na viti vya mbele katika karamu;

40  ambao hula nyumba za wajane, na kwa unafiki husali sala ndefu; hawa watapata hukumu iliyo kubwa.

41  Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi.

42  Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa.

43  Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina;

44  maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23