Marko 1
1 Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.
2 Kama ilivyoandikwa katika nabii Isaya, Tazama, namtuma mjumbe wangu Mbele ya uso wako, Atakayeitengeneza njia yako.
3 Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake.
4 Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi.
5 Wakamwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto wa Yordani, wakiziungama dhambi zao.
6 Na Yohana alikuwa amevaa singa za ngamia na mshipi wa ngozi kiunoni mwake, akala nzige na asali ya mwitu.
7 Akahubiri akisema, Yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya viatu vyake.
8 Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.
9 Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani.
10 Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake;
11 na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.
12 Mara Roho akamtoa aende nyikani.
13 Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia.
14 Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu,
15 akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.
16 Naye alipokuwa akipita kando ya bahari ya Galilaya, akamwona Simoni na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi.
17 Yesu akawaambia, Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.
18 Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.
19 Akaendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, nao pia walikuwa chomboni, wakizitengeneza nyavu zao.
20 Mara akawaita, wakamwacha baba yao Zebedayo ndani ya chombo pamoja na watu wa mshahara, wakaenda, wakamfuata.
21 Wakashika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha.
22 Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi.
23 Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti,
24 akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza?
25 Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke.
26 Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka.
27 Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii!
28 Habari zake zikaenea mara kotekote katika nchi zote kandokando ya Galilaya.
29 Na mara walipotoka katika sinagogi, walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea, pamoja na Yakobo na Yohana.
30 Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia habari zake.
31 Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia.
32 Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa hawawezi, na wenye pepo.
33 Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni.
34 Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua.
35 Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko.
36 Simoni na wenziwe wakamfuata;
37 nao walipomwona wakamwambia, Watu wote wanakutafuta.
38 Akawaambia, Twendeni mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana kwa hiyo nalitokea.
39 Akaenda akihubiri katika masinagogi yao, katika nchi yote ya Galilaya, na kutoa pepo.
40 Akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa.
41 Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika.
42 Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika.
43 Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara,
44 akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao.
45 Lakini akatoka, akaanza kuhubiri maneno mengi, na kulitangaza lile neno, hata Yesu asiweze tena kuingia mjini kwa wazi; bali alikuwako nje mahali pasipokuwa na watu, wakamwendea kutoka kila mahali.