«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Luka 3

1  Mwaka wa kumi na tano wa kutawala kwake Kaisari Tiberio, Pontio Pilato alipokuwa liwali wa Uyahudi, na Herode mfalme wa Galilaya, na Filipo, ndugu yake, mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania mfalme wa Abilene,

2  wakati wa ukuhani mkuu wa Anasi na Kayafa, neno la Mungu lilimfikia Yohana, mwana wa Zakaria, jangwani.

3  Akafika nchi yote iliyo karibu na Yordani, akihubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi,

4  kama ilivyoandikwa katika chuo cha maneno ya nabii Isaya; Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito yake.

5  Kila bonde litajazwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa; Palipopotoka patakuwa pamenyoka, Na palipoparuza patalainishwa;

6  Na wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu.

7  Basi, aliwaambia makutano ya wale waliomwendea ili awabatize, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?

8  Basi, toeni matunda yapatanayo na toba; wala msianze kusema mioyoni mwenu, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba katika mawe haya Mungu aweza kumwinulia Ibrahimu watoto.

9  Na sasa hivi shoka limekwisha kuwekwa penye mashina ya miti; basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa motoni.

10  Makutano wakamwuliza, Tufanye nini basi?

11  Akawajibu akiwaambia, Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye vivyo hivyo.

12  Watoza ushuru nao wakaja kubatizwa, wakamwuliza, Mwalimu, tufanye nini sisi?

13  Akawaambia, Msitoze kitu zaidi kuliko mlivyoamriwa.

14  Askari nao wakamwuliza, wakisema, Sisi nasi tufanye nini? Akawaambia, Msidhulumu mtu, wala msishitaki kwa uongo; tena mtoshewe na mshahara wenu.

15  Basi, watu walipokuwa wakingoja yatakayotokea, wote wakiwaza-waza mioyoni mwao habari za Yohana, kama labda yeye ndiye Kristo,

16  Yohana alijibu akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto;

17  ambaye pepeo lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake, na kuikusanya ngano ghalani mwake, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.

18  Basi, kwa maonyo mengine mengi aliwahubiri watu.

19  Lakini mfalme Herode alipokaripiwa na yeye kwa ajili ya Herodia, mke wa nduguye, na maovu yote aliyoyafanya Herode,

20  aliongeza na hili juu ya yote, alimfunga Yohana gerezani.

21  Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka;

22  Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.

23  Na Yesu mwenyewe, alipoanza kufundisha, alikuwa amepata umri wake kama miaka thelathini, akidhaniwa kuwa ni mwana wa Yusufu, wa Eli,

24  wa Mathati, wa Lawi, wa Melki, wa Yana, wa Yusufu,

25  wa Matathia, wa Amosi, wa Nahumu, wa Esli, wa Nagai,

26  wa Maathi, wa Matathia, wa Semei, wa Yusufu, wa Yuda,

27  wa Yoana, wa Resa, wa Zerubabeli, wa Shealtieli, wa Neri,

28  wa Melki, wa Adi, wa Kosamu, wa Elmadamu, wa Eri,

29  wa Yoshua, wa Eliezeri, wa Yorimu, wa Mathati, wa Lawi,

30  wa Simeoni, wa Yuda, wa Yusufu, wa Yonamu, wa Eliakimu,

31  wa Melea, wa Mena, wa Matatha, wa Nathani, wa Daudi,

32  wa Yese, wa Obedi, wa Boazi, wa Salmoni, wa Nashoni,

33  wa Aminadabu, wa Aramu, wa Hesroni, wa Peresi, wa Yuda,

34  wa Yakobo, wa Isaka, wa Ibrahimu, wa Tera, wa Nahori,

35  wa Serugi, wa Ragau, wa Pelegi, wa Eberi, wa Sala,

36  wa Kenani, wa Arfaksadi, wa Shemu, wa Nuhu, wa Lameki,

37  wa Methusela, wa Henoko, wa Yaredi, wa Mahalaleli, wa Kenani,

38  wa Enoshi, wa Sethi, wa Adamu, wa Mungu.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23