«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Luka 23

1  Wakasimama mkutano wote, wakampeleka kwa Pilato.

2  Wakaanza kumshitaki, wakisema, Tumemwona huyu akipotosha taifa letu, na kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi, akisema kwamba yeye mwenyewe ni Kristo, mfalme.

3  Pilato akamwuliza, akisema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu akamwambia, Wewe wasema.

4  Pilato akawaambia wakuu wa makuhani na makutano, Sioni neno lililo ovu katika mtu huyu.

5  Nao walikaza sana, wakisema, Huwataharakisha watu, akifundisha katika Uyahudi yote, tokea Galilaya mpaka huku.

6  Pilato aliposikia hayo aliuliza kama huyu ni mtu wa Galilaya.

7  Na alipopata habari ya kuwa yu chini ya mamlaka ya Herode, alimpeleka kwa Herode, kwa kuwa yeye naye alikuwapo Yerusalemu siku zile.

8  Na Herode alipomwona Yesu alifurahi sana, kwa sababu alikuwa akitaka sana kumwona tangu siku nyingi, maana amesikia habari zake, akataraji kuona ishara iliyofanywa na yeye.

9  Akamwuliza maneno mengi, yeye asimjibu lo lote.

10  Wakuu wa makuhani na waandishi wakasimama wakamshitaki kwa nguvu sana.

11  Basi Herode akamfanya duni, pamoja na askari zake, akamdhihaki, na kumvika mavazi mazuri; kisha akamrudisha kwa Pilato.

12  Basi siku ile ile Herode na Pilato walipatana kwa urafiki kwa maana hapo kwanza walikuwa na uadui wao kwa wao.

13  Na Pilato akawakutanisha wakuu wa makuhani, na wakubwa, na watu,

14  akawaambia, Mtu huyu mmemleta kwangu kana kwamba anapotosha watu; nami, tazama, nimeamua mambo yake mbele yenu, ila sikuona kwake kosa lo lote katika mambo hayo mliyomshitaki;

15  wala hata Herode, kwa maana amemrudisha kwetu; basi tazama, hakuna neno lo lote alilolitenda lipasalo kufa.

16  Kwa hiyo nitamrudi, kisha nitamfungua. [

17  Maana ilimlazimu kuwafungulia mfungwa mmoja wakati wa sikukuu.]

18  Wakapiga kelele wote pamoja, wakisema, Mwondoe huyu, utufungulie Baraba.

19  Naye ni mtu aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina iliyotokea mjini, na kwa uuaji

20  Basi Pilato alisema nao mara ya pili, kwa vile alivyotaka kumfungua Yesu.

21  Lakini wakapiga kelele, wakisema, Msulibishe. Msulibishe.

22  Akawaambia mara ya tatu, Kwa sababu gani? Huyu ametenda uovu gani? Sikuona kwake hata neno lipasalo kufa. Basi nikiisha kumrudi nitamfungua.

23  Lakini wakatoa sauti zao kwa nguvu sana, wakitaka asulibiwe. Sauti zao zikashinda.

24  Pilato akahukumu kwamba haja yao ifanyike.

25  Akamfungua yule aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina na uuaji, yule waliyemtaka, akamtoa Yesu wamfanyie watakavyo.

26  Na walipokuwa wakimwondoa walimkamata mtu mmoja, Simoni Mkirene, aliyekuwa ametoka shamba, wakamtwika msalaba, auchukue nyuma yake Yesu.

27  Mkutano mkubwa wa watu wakamfuata, na wanawake waliokuwa wakijipiga vifua na kumwombolezea.

28  Yesu akawageukia, akasema, Enyi binti za Yerusalemu, msinililie mimi, bali jililieni nafsi zenu na watoto wenu.

29  Kwa maana tazama, siku zitakuja watakaposema, Heri walio tasa, na matumbo yasiyozaa, na maziwa yasiyonyonyesha.

30  Ndipo watakapoanza kuiambia milima, Tuangukieni, na vilima, Tufunikeni.

31  Kwa kuwa kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

32  Wakapelekwa na wawili wengine, wahalifu, wauawe pamoja naye.

33  Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto.

34  Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura.

35  Watu wakasimama wakitazama. Wale wakuu nao walikuwa wakimfanyia mzaha, wakisema, Aliokoa wengine; na ajiokoe mwenyewe, kama ndiye Kristo wa Mungu, mteule wake.

36  Wale askari nao wakamfanyia dhihaka, wakimwendea na kumletea siki,

37  huku wakisema, Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujiokoe mwenyewe.

38  Na juu yake palikuwa na anwani; HUYU NDIYE MFALME WA WAYAHUDI.

39  Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.

40  Lakini yule wa pili akamjibu akamkemea, akisema, Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo?

41  Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lo lote lisilofaa.

42  Kisha akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.

43  Yesu akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi.

44  Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda,

45  jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati.

46  Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.

47  Alipokwisha kusema hayo alikata roho. Yule akida alipoona yaliyotukia, alimtukuza Mungu, akisema, Hakika yake, mtu huyu alikuwa mwenye haki.

48  Na makutano yote ya watu waliokuwa wamekutanika kutazama mambo hayo, walipoona yaliyotendeka, wakaenda zao kwao, wakijipiga-piga vifua.

49  Na wote waliojuana naye, na wale wanawake walioandamana naye toka Galilaya, wakasimama kwa mbali, wakitazama mambo hayo.

50  Na tazama, akatoka mtu mmoja, jina lake Yusufu, ambaye ni mtu wa baraza, mtu mwema, mwenye haki;

51  (wala hakulikubali shauri na tendo lao), naye ni mtu wa Arimathaya, mji mmoja wa Wayahudi, tena anautazamia ufalme wa Mungu;

52  mtu huyo alikwenda kwa Pilato, akataka kupewa mwili wa Yesu.

53  Akaushusha, akauzinga sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililochongwa mwambani, ambalo hajalazwa mtu bado ndani yake.

54  Na siku ile ilikuwa siku ya Maandalio, na sabato ikaanza kuingia.

55  Na wale wanawake waliokuja naye toka Galilaya walifuata, wakaliona kaburi, na jinsi mwili wake ulivyowekwa.

56  Wakarudi, wakafanya tayari manukato na marhamu. Na siku ya sabato walistarehe kama ilivyoamriwa.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23