«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Mambo ya Walawi 21

1  Kisha Bwana akamwambia Musa, Nena na hao makuhani, wana wa Haruni, uwaambie, Mtu asijinajisi kwa ajili ya wafu katika watu wake;

2  isipokuwa ni kwa ajili ya jamaa yake wa karibu, kwa ajili ya mama yake, na kwa ajili baba yake, na kwa ajili ya mwanawe, na kwa ajili ya binti yake, na kwa ajili ya nduguye mwanamume;

3  na kwa ajili ya umbu lake aliye mwanamwali, aliye wa udugu kwake, ambaye hajaolewa na mume; ana ruhusa kujitia unajisi kwa ajili yake huyo.

4  Asijitie unajisi, ijapokuwa ni mkubwa katika watu wake, hata akajinajisi.

5  Wasijifanyie upaa kichwani, wala wasinyoe pembe za ndevu zao, wala wasichanje chale katika miili yao.

6  Watakuwa watakatifu kwa Mungu wao, wala wasilinajisi jina la Mungu wao; kwa kuwa wao ndio wasongezao sadaka za Bwana kwa njia ya moto, chakula cha Mungu wao; kwa ajili ya hayo watakuwa watakatifu.

7  Wasimwoe mwanamke aliye kahaba, au huyo aliye mwenye unajisi; wala wasimwoe mwanamke aliyeachwa na mumewe; kwa kuwa yeye kuhani ni mtakatifu kwa Mungu wake.

8  Kwa hiyo basi utamtakasa; kwa kuwa yeye husongeza chakula cha Mungu wako; atakuwa mtakatifu kwako wewe; kwa kuwa mimi Bwana niwatakasaye ninyi ni mtakatifu.

9  Na binti ya kuhani ye yote atakapojitia unajisi kwa ukahaba, amemtia unajisi baba yake; atachomwa moto.

10  Na yeye aliye kuhani mkuu katika nduguze, ambaye mafuta ya kutiwa yamemiminwa kichwani mwake, naye akawekwa wakfu ili ayavae hayo mavazi, yeye hataziacha wazi nywele za kichwa chake, wala hatazirarua nguo zake;

11  wala hataingia penye maiti, wala asijitie unajisi kwa ajili ya baba yake wala mama yake;

12  wala asitoke katika mahali patakatifu, wala asipatie unajisi mahali patakatifu pa Mungu wake; kwa kuwa utakaso wa hayo mafuta ya kutiwa ya Mungu wake u juu yake; mimi ndimi Bwana.

13  Naye atamwoa mwanamke katika ubikira wake.

14  Asitwae mjane, wala mwanamke aliyeachwa na mumewe, wala mwanamke mwenye unajisi, wala kahaba; lakini atamwoa mwanamwali katika watu wake mwenyewe.

15  Naye asiwatie unajisi kizazi chake katika watu wake; kwa kuwa mimi ndimi Bwana nimtakasaye.

16  Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,

17  Nena na Haruni, umwambie, Mtu awaye yote wa kizazi chako wewe katika vizazi vyao, aliye na kilema, asikaribie kusongeza chakula cha Mungu wake.

18  Kwa kuwa mtu awaye yote aliye na kilema hatakaribia; mtu kipofu, au kiwete, au mtu aliye na pua iliyoharibika, au aliye na kitu kilichozidi vimpasavyo mwili,

19  au mtu aliyevunjika mguu, au aliyevunjika mkono,

20  au aliye na kijongo, au aliye kibeti, au aliye na kilema cha jichoni, au aliye na upele, au mwenye buba, au aliyevunjika mapumbu;

21  mtu awaye yote wa kizazi cha Haruni kuhani aliye na kilema asikaribie kuzisongeza sadaka za Bwana kwa njia ya moto; ana kilema huyo asikaribie kusongeza chakula cha Mungu wake.

22  Atakula chakula cha Mungu wake, katika hicho kilicho kitakatifu sana, na hicho kilicho kitakatifu.

23  Lakini hataingia ndani ya pazia, wala asikaribie madhabahu, kwa sababu ana kilema; ili kwamba asipanajisi patakatifu pangu; kwa kuwa mimi ndimi Bwana niwatakasaye.

24  Basi Musa akanena na Haruni na wanawe, na wana wa Israeli wote.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23