Mambo ya Walawi 19
1 Bwana akanena na Musa, akamwambia,
2 Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu.
3 Kila mtu na amche mama yake, na baba yake, nanyi mtazitunza Sabato zangu; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
4 Msigeuke kuandama sanamu, wala msijifanyizie miungu ya kusubu mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
5 Nanyi hapo mtakapomchinjia Bwana sadaka ya amani mtaisongeza ili kwamba mpate kukubaliwa.
6 Italiwa siku iyo hiyo mliyoichinja, na siku ya pili yake; na kama kitu cho chote katika sadaka hiyo kilisalia hata siku ya tatu kitachomwa moto.
7 Kwamba sadaka hiyo yaliwa hata kidogo siku ya tatu ni machukizo; haitakubaliwa;
8 lakini kila mtu atakayekula atauchukua uovu wake mwenyewe, kwa sababu amekinajisi kitu hicho kitakatifu cha Bwana; na nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake.
9 Na mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa kabisa pembe za shamba lako, wala usiyakusanye masazo ya mavuno yako;
10 wala usiyakusanye masazo ya mizabibu yako, wala usiyaokote matunda ya mizabibu yako yaliyopukutika; uyaache kwa ajili ya maskini na mgeni; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
11 Msiibe, wala msidanganye, wala msiambiane uongo.
12 Msiape uongo kwa jina langu, hata ukalinajisi jina la Mungu wako; Mimi ndimi Bwana.
13 Usimdhulumu jirani yako, wala kumnyang'anya mali yake; ijara yake aliyeajiriwa isikae kwako usiku kucha hata asubuhi.
14 Usimlaani kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; Mimi ndimi Bwana.
15 Msitende yasiyo haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki.
16 Usiende huko na huko katikati ya watu wako, kama mchongezi; wala usisimame kinyume cha damu ya jirani yako; mimi ndimi Bwana.
17 Usimchukie ndugu yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, wala usichukue dhambi kwa ajili yake.
18 Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi Bwana.
19 Mtazishika amri zangu. Usiwaache wanyama wako wa mfugo wakazaana kwa namna mbalimbali; usipande shamba lako mbegu za namna mbili pamoja; wala usivae mwilini mwako nguo ya namna mbili zilizochanganywa pamoja.
20 Tena mtu ye yote alalaye na mwanamke aliye mjakazi, naye ameposwa na mume, wala hakukombolewa kwa lo lote, wala hakupewa uhuru; wataadhibiwa; hawatauawa, kwa sababu huyo mwanamke hakuwa huru.
21 Na huyo mume ataleta sadaka yake ya hatia aitoe kwa Bwana, hata mlangoni pa hema ya kukutania; kondoo mume kwa hiyo sadaka ya hatia.
22 Kisha huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, kwa huyo kondoo mume wa sadaka ya hatia mbele za Bwana, kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya; naye atasamehewa hiyo dhambi yake aliyoifanya.
23 Nanyi hapo mtakapoingia nchi ile, mkiwa mmepanda miti ya namna zote kwa ajili ya chakula, ndipo mtayahesabu matunda yake kama ni kutotahiriwa; muda wa miaka mitatu miti hiyo itakuwa kwenu kama kutotahiriwa; matunda yake hayataliwa.
24 Lakini mwaka wa nne matunda yake yote yatakuwa ni matakatifu, kwa ajili ya kumpa Bwana shukrani.
25 Na katika mwaka wa tano mtakula katika matunda yake, ili ipate kuwapa maongeo yake; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
26 Msile kitu cho chote pamoja na damu yake; wala msifanye kuloga, wala kutumia utambuzi.
27 Msinyoe denge pembe za vichwani, wala msiharibu pembe za ndevu zenu.
28 Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi Bwana.
29 Usimnajisi binti yako, ili kumfanya awe kahaba; isiwe hiyo nchi kuuandama ukahaba, na nchi kujawa na uovu mkuu.
30 Zishikeni Sabato zangu, mpaheshimu patakatifu pangu; mimi ndimi Bwana.
31 Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
32 Mwondokeeni mtu mwenye mvi; heshimuni uso wa mtu mzee; nawe mche Mungu wako, Mimi ndimi Bwana.
33 Na mgeni akikaa pamoja nawe katika nchi yako, usimdhulumu.
34 Mgeni akaaye pamoja nawe atakuwa kama mzalia kwenu; mpende kama nafsi yako; kwa maana ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri; Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
35 Msifanye yasiyo haki katika hukumu, wala katika kupima, wala katika mizani, wala katika cheo.
36 Mizani ya haki, vipimo vya haki, efa ya haki, hini ya haki, ndivyo mtakavyokuwa navyo. Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, niliyewatoa katika nchi ya Misri.
37 Zishikeni sheria zangu, na hukumu zangu, na kuzitenda. Mimi ndimi Bwana.