Mambo ya Walawi 18
1 Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Nena wewe na wana wa Israeli, uwaambie, Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
3 Nanyi msifanye matendo kama yale ya nchi ya Misri mliyokaa; wala msifanye matendo kama yale ya nchi ya Kanaani, nitakayowapeleka; wala msiende katika amri zao hao.
4 Mtazifanya hukumu zangu, nanyi mtazishika amri zangu, ili mwenende katika hizo; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
5 Kwa ajili ya hayo mtazishika amri zangu na hukumu zangu; ambazo mtu akizitumia ataishi kwa hizo; mimi ndimi Bwana.
6 Mtu ye yote aliye wa kwenu asimkaribie mwenziwe aliye wa jamaa yake ya karibu ili kumfunua utupu; mimi ndimi Bwana.
7 Utupu wa baba yako, wala utupu wa mama yako, usifunue, maana ndiye mama yako; usifunue utupu wake.
8 Utupu wa mke wa baba yako, usifunue; maana, ni utupu wa baba yako.
9 Utupu wa umbu lako, binti ya baba yako, au binti ya mama yako, kwamba alizaliwa nyumbani mwenu au kwamba alizaliwa kwengine, utupu wa hao usifunue.
10 Utupu wa binti ya mwanao mume, au wa binti ya binti yako, utupu wao hao usifunue; kwa kuwa ndio utupu wako mwenyewe.
11 Utupu wa binti ya mkewe baba yako, aliyezaliwa na baba yako, yeye ni umbu lako, usifunue utupu wake.
12 Usifunue utupu wa umbu lake baba yako; maana, yeye ni jamaa aliye karibu.
13 Usifunue utupu wa umbu la mama yako; maana, yeye ni jamaa ya mama yako ya karibu.
14 Usifunue utupu wa ndugu ya baba yako, usimkaribie mkewe huyo; yeye ni shangazi lako.
15 Usifunue utupu wa mkweo mwanamke; yeye ni mke wa mwanao; usifunue utupu wake huyo.
16 Usifunue utupu wa mke wa nduguyo; maana, ni utupu wa nduguyo.
17 Usifunue utupu wa mwanamke na binti yake; usimtwae binti ya mwanawe mume, au binti ya binti yake, ili kufunua utupu wake; hao ni jamaa ya karibu; ni uovu mkuu.
18 Wala usitwae mwanamke pamoja na nduguye, awe mtesi wake, na kufunua utupu wake, huyo wa pili atakapokuwa yu hai.
19 Nawe usimkaribie mwanamke kufunua utupu wake wakati wa kutengwa kwa ajili ya unajisi wake.
20 Usilale na mke wa mwenzio, ukajitia unajisi naye.
21 Nawe usitoe kizazi chako cho chote na kuwapisha kwa Moleki, wala usilinajisi jina la Mungu wako; mimi ndimi Bwana.
22 Usilale na mwanamume mfano wa kulala na mwanamke; ni machukizo.
23 Wala usilale na mnyama ye yote, ili kujitia unajisi kwake; wala mwanamke asisimame mbele ya mnyama ili kulala naye; ni uchafuko.
24 Msijitie unajisi katika mambo hayo hata mojawapo; kwa maana hizo taifa nitakazozitoa mbele zenu zimekuwa najisi kwa mambo hayo yote;
25 na hiyo nchi imekuwa najisi; kwa ajili ya hayo naipatiliza uovu wake juu yake, na hiyo nchi yatapika wenyeji wake na kuwatoa.
26 Kwa hiyo mtazishika amri zangu na hukumu zangu, wala msifanye machukizo hayo mojawapo; yeye aliye mzalia, wala mgeni aketiye kati yenu;
27 (kwa kuwa hao watu wa nchi wameyafanya machukizo haya yote, hao waliotangulia mbele zenu, na hiyo nchi imekuwa najisi;)
28 ili kwamba hiyo nchi isiwatapike na ninyi pia, hapo mtakapoitia unajisi, kama ilivyoitapika hiyo taifa iliyotangulia mbele yenu.
29 Kwani mtu awaye yote atakayefanya machukizo hayo mojawapo, nafsi hizo zitakazoyafanya zitakatiliwa mbali na watu wao.
30 Kwa ajili ya hayo yashikeni mausia yangu, ili kwamba msifanye kabisa desturi hizi zichukizazo mojawapo, zilizotangulia kufanywa mbele zenu, wala msijitie unajisi katika mambo hayo; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.