«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Maombolezo 5

1  Ee Bwana, kumbuka yaliyotupata; Utazame na kuiona aibu yetu.

2  Urithi wetu umegeuka kuwa mali ya wageni; Na nyumba zetu kuwa mali ya makafiri.

3  Tumekuwa yatima waliofiwa na baba; Mama zetu wamekuwa kama wajane.

4  Tumekunywa maji yetu kwa fedha; Kuni zetu twauziwa.

5  Watufuatiao wa juu ya shingo zetu; Tumechoka tusipate raha yo yote.

6  Tumewapa hao Wamisri mkono; Na Waashuri nao, ili tushibe chakula.

7  Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao.

8  Watumwa wanatutawala; Hakuna mtu wa kutuokoa na mikono yao.

9  Twapata chakula kwa kujihatarisha nafsi zetu; Kwa sababu ya upanga wa nyikani.

10  Ngozi yetu ni nyeusi kama tanuu; Kwa sababu ya hari ya njaa ituteketezayo.

11  Huwatia jeuri wanawake katika Sayuni; Na mabikira katika miji ya Yuda.

12  Wakuu hutungikwa kwa mikono yao; Nyuso za wazee hazipewi heshima.

13  Vijana huyachukua mawe ya kusagia; Na watoto hujikwaa chini ya kuni.

14  Wazee wameacha kwenda langoni; Na vijana kwenda ngomani.

15  Furaha ya mioyo yetu imekoma; Machezo yetu yamegeuka maombolezo.

16  Taji ya kichwa chetu imeanguka; Ole wetu! Kwa kuwa tumetenda dhambi.

17  Kwa sababu hiyo mioyo yetu imezimia; Kwa ajili ya hayo macho yetu hayaoni vema.

18  Kwa ajili ya mlima Sayuni ulio ukiwa, Mbweha hutembea juu yake.

19  Wewe, Bwana, unadumu milele; Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi.

20  Mbona watusahau sikuzote; Na kutuacha muda huu mwingi?

21  Ee Bwana, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.

22  Isipokuwa wewe umetukataa kabisa; Nawe una hasira nyingi sana juu yetu.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23