Waamuzi 17
1 Wakati huo alikuwako mtu mmoja wa nchi ya vilima ya Efraimu, ambaye jina lake alikuwa akiitwa Mika.
2 Naye akamwambia mama yake, Hizo fedha elfu na mia moja ulizonyang'anywa, ambazo uliweka kiapo kwa ajili yake na kusema masikioni mwangu, tazama, ninazo mimi hizo fedha; ni mimi niliyezitwaa. Mama yake akasema, mwanangu na abarikiwe na Bwana.
3 Basi akamrudishia mama yake hizo fedha elfu na mia moja. Mama yake akasema, Mimi naziweka fedha hizi kabisa ziwe wakfu kwa Bwana, zitoke mkononi mwangu kwa ajili ya mwanangu, ili kufanya sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu; basi kwa hiyo nakurudishia wewe.
4 Basi hapo alipomrudishia mama yake hizo fedha, mama yake akatwaa fedha mia mbili, akampa fundi mwenye kusubu fedha, naye akafanya sanamu ya kuchonga kwazo, na sanamu ya kusubu; ambazo zilikuwa ndani ya nyumba ya Mika.
5 Basi mtu huyo Mika alikuwa na nyumba ya miungu, naye akafanya naivera, na kinyago, akamweka wakfu mmoja miongoni mwa wanawe, akawa kuhani wake.
6 Siku hizo hapakuwa na mfalme katika israeli; kila mtu alifanya hayo aliyoyaona kuwa ni mema machoni pake mwenyewe.
7 Alikuwako mtu mmoja hirimu aliyetoka Bethlehemu-yuda, wa jamaa ya Yuda, aliyekuwa ni Mlawi, naye akakaa huko hali ya ugeni.
8 Mtu huyo akatoka katika huo mji, katika Bethlehemu-yuda, ili aende kukaa hali ya ugeni hapo atakapoona mahali; akafikilia nchi ya vilima vilima ya Efraimu katika safari yake, hata nyumba ya huyo Mika.
9 Mika akamwuliza, Watoka wapi wewe? Akamwambia, Mimi ni Mlawi wa Bethlehemu-yuda, nami naenda kukaa hali ya ugeni po pote nitakapoona mahali.
10 Mika akamwambia, kaa pamoja nami, uwe kwangu baba, tena kuhani, nami nitakupa fedha kumi mwaka kwa mwaka, na nguo ya kuvaa, na vyakula. Basi huyo Mlawi akaingia ndani.
11 Huyo Mlawi aliridhika kukaa na mtu huyo; kisha huyo hirimu akawa kwake kama wanawe mmojawapo.
12 Basi Mika akamweka wakfu huyo Mlawi, huyo hirimu, naye akawa kuhani wake, akakaa nyumbani mwa Mika.
13 Ndipo Mika akasema, Sasa najua ya kwamba Bwana atanitendea mema, kwa kuwa nina Mlawi kuwa kuhani wangu.