Waamuzi 15
1 Lakini ikawa baadaye, wakati wa mavuno ya ngano Samsoni akaenda kumtazama mkewe, akamchukulia mwana-mbuzi; akasema, Nitaingia chumbani kwa mke wangu. Lakini baba yake mwanamke hakumwacha kuingia.
2 Baba yake akasema, Hakika mimi nalidhani ya kuwa umemchukia kabisa; basi nalimpa rafiki yako. Je! Ndugu yake mdogo mzuri kuliko yeye? Tafadhali, mtwae huyo badala yake.
3 Samsoni akasema, Safari hii nitakuwa sina hatia katika habari za hawa Wafilisti, hapo nitakapowadhuru.
4 Samsoni akaenda akakamata mbweha mia tatu; kisha akatwaa vienge vya moto akawafunga mbweha mkia kwa mkia, akatia kienge kati ya kila mikia miwili.
5 Alipokwisha kuviwasha moto vile vienge, akawaachia mbweha kati ya ngano ya Wafilisti, akayateketeza matita, na ngano, hata na mashamba ya mizeituni.
6 Ndipo Wafilisti wakasema, Ni nani aliyetenda hivi? Wakasema, Ni huyo Samsoni, mkwewe yule Mtimna, kwa sababu alimchukua mkewe akampa mwenzake. Wafilisti wakaenda wakamteketeza yeye na baba yake kwa moto.
7 Samsoni akawaambia, Ikiwa ninyi mnafanya mambo kama hayo, hakika nitajilipiza kisasi juu yenu, na baadaye nitakoma.
8 Akawapiga upeo, mapigo makuu sana, kisha akatelemka akakaa katika ufa wa jabali la Etamu.
9 Basi Wafilisti wakapanda wakapiga kambi yao katika Yuda, wakajieneza katika Lehi.
10 Watu wa Yuda wakasema, Mbona mmekuja kupigana nasi? Wakasema, Tumepanda ili kumfunga Samsoni, kumtenda yeye kama alivyotutenda sisi.
11 Ndipo watu elfu tatu wa Yuda wakatelemka hata ule ufa wa jabali la Etamu, wakamwambia Samsoni, Je! Hujui ya kuwa Wafilisti wanatutawala? Ni nini hii, basi, uliyotutenda? Akawaambia, Kadiri ile walivyonitenda mimi, ndivyo nilivyowatenda wao.
12 Wakamwambia, Tumeshuka ili kukufunga, tupate kukutia katika mikono ya Wafilisti. Samsoni akawaambia, Niapieni ya kwamba ninyi wenyewe hamtaniangukia.
13 Wakamwambia, wakisema, Vema, lakini tutakufunga sana, na kukutia katika mikono yao; lakini hakika hatutakuua. Basi wakamfunga kwa kamba mbili mpya, wakamchukua kutoka huko jabalini.
14 Alipofika Lehi, Wafilisti wakapiga kelele walipokutana naye; ndipo roho ya Bwana ikamjia kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake zikawa kama kitani iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake vikaanguka mikononi mwake.
15 Naye akaona mfupa mbichi wa taya ya punda, akautwaa, akapiga watu elfu kwa mfupa huo;
16 Samsoni akasema, Kwa taya ya punda chungu juu ya chungu, Kwa taya ya punda nimepiga watu elfu.
17 Ikawa, alipokuwa amekwisha kunena akautupa ule mfupa wa taya mkononi mwake; na mahali pale pakaitwa Ramath-lehi.
18 Kisha akaona kiu sana, akamwita Bwana akasema, Wewe umetupa wokovu huu kwa mkono wa mtumishi wako; na sasa nitakufa kwa kiu, na kuanguka katika mikono ya watu wasiotahiriwa.
19 Lakini Mungu akapasua mahali penye shimo palipo katika Lehi, pakatoka maji; naye alipokwisha kunywa, roho yake ikamrudia, akaburudika; kwa hiyo jina la mahali pale likaitwa Enhakore,
20 Naye akawa mwamuzi wa Israeli: katika siku za Wafilisti muda wa miaka ishirini.