Yoshua 6
1 Basi Yeriko ulikuwa umefungwa kabisa kwa sababu ya wana wa Israeli; hapana mtu aliyetoka wala hapana mtu aliyeingia.
2 Bwana akamwambia Yoshua, Tazama, nimeutia Yeriko katika mkono wako, na mfalme wake, na mashujaa wake.
3 Nanyi mtauzunguka mji huu, watu wote wa vita, mkiuzunguka mji mara moja. Fanya hivi siku sita.
4 Na makuhani saba watachukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume, mbele ya hilo sanduku; na siku ya saba mtauzunguka mji mara saba, nao makuhani watapiga tarumbeta zao.
5 Kisha itakuwa watakapopiga hizo pembe za kondoo waume kwa nguvu, nanyi mtakaposikia sauti ya tarumbeta, watu wote watapiga kelele kwa sauti kuu; na ukuta wa mji utaanguka chini pale pale, na hao watu watapanda, kila mtu akiendelea mbele kukabili.
6 Bali Yoshua, mwana wa Nuni, akawaita makuhani, akawaambia, Lichukueni sanduku la agano, tena makuhani saba na wachukue tarumbeta saba za pembe za kondoo waume mbele ya sanduku la Bwana.
7 Naye akawaambia watu, Piteni mbele, mkauzunguke mji, na hao watu wenye silaha na watangulie mbele ya sanduku la Bwana.
8 Basi ikawa Yoshua alipokwisha kusema na watu, wale makuhani saba, wenye kuzichukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume mbele za Bwana, wakatangulia, wakazipiga hizo tarumbeta; nalo sanduku la agano la Bwana likawafuata.
9 Wale watu wenye silaha walikwenda mbele ya hao makuhani waliozipiga tarumbeta, na wale waliokuwa nyuma wakalifuata hilo sanduku; makuhani wakizipiga tarumbeta walipokuwa wakienda.
10 Yoshua akawaamuru watu, akasema Msipige kelele, wala sauti zenu zisisikiwe, wala neno lo lote lisitoke kinywani mwenu, hata siku ile nitakapowaamuru kupiga kelele, ndipo mtakapopiga kelele.
11 Basi akalipeleka sanduku la Bwana liuzunguke huo mji, likauzunguka mara moja, kisha wakaenda kambini wakakaa kambini.
12 Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, nao makuhani wakalichukua sanduku la Bwana.
13 Na wale makuhani saba wakazichukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume mbele ya sanduku la Bwana, wakaendelea wakazipiga tarumbeta; nao watu wenye silaha wakawatangulia, na hao waliokuwa nyuma wakalifuata sanduku la Bwana; makuhani wakizipiga tarumbeta walipokuwa wakienda.
14 Siku ya pili wakauzunguka mji mara moja, wakarejea kambini; ndivyo walivyofanya siku sita.
15 Ikawa siku ya saba wakaondoka asubuhi na mapema wakati wa mapambazuko, wakauzunguka mji vivyo hivyo mara saba; ila siku hiyo waliuzunguka huo mji mara saba.
16 Hata mara ya saba makuhani walipozipiga tarumbeta, Yoshua akawaambia watu, Pigeni kelele; kwa maana Bwana amewapeni mji huu.
17 Na mji huu utakuwa wakfu kwa Bwana, mji wenyewe na vitu vyote vilivyomo; isipokuwa Rahabu, yule kahaba, ataishi, yeye na watu wote walio pamoja naye nyumbani, kwa sababu aliwaficha hao wapelelezi tuliowatuma.
18 Na ninyi, msikose kujiepusha na kitu kilichowekwa wakfu; msije mkakitwaa kitu kilichowekwa wakfu, baada ya kukiweka wakfu; nanyi hivyo mtayafanya matuo ya Israeli kuwa yamelaaniwa na kuyafadhaisha.
19 Lakini fedha yote, na dhahabu, na vyombo vya shaba, na chuma, ni vitakatifu kwa Bwana; vitaletwa katika hazina ya Bwana.
20 Basi watu wakapiga kelele, na makuhani wakazipiga tarumbeta; hata ikawa, hapo watu waliposikia sauti ya tarumbeta hao watu wakapiga kelele kwa sauti kuu sana, na ule ukuta wa mji ukaanguka nchi kabisa, hata watu wakapanda juu, wakaingia katika mji, kila mtu akiendelea kukabili mbele; wakautwaa huo mji.
21 Basi wakaangamiza kabisa vitu vyote vilivyokuwa ndani ya mji, wanaume na wanawake, watoto na wazee, na ng'ombe, na kondoo, na punda, kwa makali ya upanga.
22 Naye Yoshua akawaambia wale wanaume wawili walioipeleleza nchi, Ingieni katika nyumba ya yule kahaba, mkamtoe huyo mwanamke mwenyewe na vitu vyote alivyo navyo, kama mlivyomwapia.
23 Basi wale vijana wapelelezi wakaingia, wakamtoa Rahabu, na baba yake, na mama yake, na ndugu zake, na vitu vyote walivyokuwa navyo, wakawatoa na jamaa zake wote pia; wakawaweka nje ya matuo ya Israeli.
24 Kisha wakauteketeza mji kwa moto, na vitu vyote vilivyokuwa ndani yake; bali fedha, na dhahabu, na vyombo vya shaba, na vya chuma, wakavitia katika hazina ya nyumba ya Bwana.
25 Lakini Yoshua akamhifadhi Rahabu, yule kahaba, na watu wa nyumba ya baba yake, na vitu vyote alivyokuwa navyo; naye akakaa kati ya Israeli hata leo; kwa sababu aliwaficha wale wajumbe aliowatuma Yoshua ili kuupeleleza mji wa Yeriko.
26 Naye Yoshua akawaapisha kiapo wakati ule, akasema, Na alaaniwe mbele za Bwana mtu yule atakayeinuka na kuujenga tena mji huu wa Yeriko; ataweka msingi wake kwa kufiliwa na mzaliwa wa kwanza wake, tena atayasimamisha malango yake kwa kufiliwa na mtoto wake mwanamume aliye mdogo.
27 Basi Bwana alikuwa pamoja na Yoshua; sifa zake zikaenea katika nchi ile yote.