«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Yoshua 23

1  Hata ikawa baada ya siku nyingi, Bwana alipokuwa amekwisha kuwapa Israeli raha mbele ya adui zao pande zote, naye Yoshua alipokuwa mzee, mwenye miaka mingi sana,

2  Yoshua akawaita Israeli wote, wazee wao, na wakuu wao, na makadhi yao, na maakida yao, akawaambia, Mimi ni mzee, nami nimekwendelea sana katika miaka yangu;

3  nanyi mmeona mambo yote ambayo Bwana, Mungu wenu, amewatenda mataifa haya yote kwa ajili yenu; kwa maana Bwana, Mungu wenu, ndiye aliyewapigania ninyi.

4  Tazama, nimewagawieni kwa kura mataifa haya yaliyobaki, yawe urithi kwa kabila zenu, toka mto wa Yordani, pamoja na mataifa yote niliyowakatilia mbali, mpaka bahari kubwa upande wa machweo ya jua.

5  Yeye Bwana, Mungu wenu, atawatoa kwa nguvu mbele yenu, atawafukuza wasiwe mbele ya macho yenu tena; nanyi mtaimiliki nchi yao, kama Bwana Mungu wenu, alivyowaambia.

6  Basi, iweni mashujaa sana kuyashika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati ya Musa, na kuyatenda, msiyaache kwa kugeukia upande wa kuume wala upande wa kushoto.

7  Msiingie kati ya mataifa haya, yaani, haya yaliyobaki kati yenu; wala msitaje majina ya miungu yao, wala kuwaapisha watu kwa majina hayo, wala kuitumikia, wala kujiinamisha mbele yao;

8  bali shikamaneni na Bwana, Mungu wenu, kama mlivyotenda hata hivi leo.

9  Maana Bwana amefukuza mbele yenu mataifa walio hodari, kisha wenye nguvu, lakini kwenu ninyi hapana mtu aliyesimama mbele yenu hata leo.

10  Mtu mmoja miongoni mwenu atafukuza watu elfu; maana Bwana, Mungu wenu, ndiye anayewapigania, kama alivyowaambia.

11  Jihadharini nafsi zenu, basi, ili mmpende Bwana, Mungu wenu.

12  Lakini mkirudi nyuma kwa njia yo yote na kushikamana na mabaki ya mataifa, yaani, mataifa haya yaliyobaki kati yenu, na kuoana nao, na kuingia kwao, nao kuingia kwenu;

13  jueni hakika ya kuwa Bwana, Mungu wenu, hatawafukuza tena mataifa haya mbele ya macho yenu, bali watakuwa mtego kwenu na tanzi, na mjeledi mbavuni mwenu, na miiba machoni mwenu, hata mtakapoangamia na kutoka katika nchi hii njema, ambayo Bwana, Mungu wenu, amewapa ninyi.

14  Angalieni, mimi leo ninakwenda njia ile waendayo watu wote wa ulimwengu; nanyi nyote mnajua mioyoni mwenu, na rohoni mwenu, ya kuwa halikuwapungukia ninyi hata neno moja katika mambo hayo mema yote aliyoyanena Bwana, Mungu wenu, katika habari zenu; yote yametimia kwenu hapana neno lo lote mlilopungukiwa.

15  Kisha itakuwa, kama yalivyowafikilia yale mambo mema yote, Bwana, Mungu wenu, aliyowaahidia ninyi, kadhalika Bwana atawafikilizia mabaya yote, hata atakapokuwa amewaangamiza katika nchi hii njema, Bwana Mungu wenu, aliyowapa.

16  Hapo mtakapolivunja agano la Bwana, Mungu wenu, alilowaamuru, na kwenda kuitumikia miungu mingine, na kujiinamisha mbele yao, ndipo hasira ya Bwana itakapowaka juu yenu, nanyi mtaangamia upesi katika nchi hii njema aliyowapa.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23