Yoeli 3
1 Kwa maana, angalieni, siku zile, na wakati ule, nitakapowarudisha mateka wa Yuda na Yerusalemu,
2 nitakusanya mataifa yote, nami nitawaleta chini katika bonde la Yehoshafau, na huko nitawahukumu kwa ajili ya watu wangu, na kwa ajili ya urithi wangu, Israeli, ambao wamewatawanya kati ya mataifa, na kuigawanya nchi yangu.
3 Nao wamewapigia kura watu wangu; na mtoto mwanamume wamemtoa ili kupata kahaba, na mtoto mwanamke wamemwuza ili kupata divai, wapate kunywa.
4 Naam, na ninyi ni kitu gani kwangu, enyi Tiro, na Sidoni, na nchi zote za Filisti? Je! Mtanirudishia malipo? Au mtanitenda neno lo lote? Upesi na kwa haraka nitawarudishia malipo yenu juu ya vichwa vyenu wenyewe.
5 Kwa kuwa mmetwaa fedha yangu na dhahabu yangu, nanyi mmevichukua vitu vyangu vyema vipendezavyo, na kuviingiza katika hekalu zenu;
6 tena watoto wa Yuda na watoto wa Yerusalemu mmewauzia Wayunani, mpate kuwahamisha mbali na mipaka yao;
7 tazameni, nitawaamsha wapatoke mahali mlipowauza, nami nitawarudishia malipo yenu juu ya vichwa vyenu wenyewe.
8 Na mimi nitawauza wana wenu na binti zenu, na kuwatia katika mikono ya wana wa Yuda, nao watawauzia watu wa Sheba, taifa lililo mbali kabisa; kwa maana Bwana ndiye aliyesema neno hili.
9 Tangazeni haya kati ya mataifa; takaseni vita; waamsheni mashujaa; watu wa vita na wakaribie; na wapande juu.
10 Yafueni majembe yenu yawe panga, na miundu yenu iwe mikuki; aliye dhaifu na aseme, Mimi ni hodari.
11 Fanyeni haraka, mje, enyi mataifa yote, wa pande zote, jikusanyeni pamoja; na huko watelemshe mashujaa wako wote, Ee Bwana.
12 Mataifa na wajihimize, wakapande juu katika bonde la Yehoshafau; maana huko ndiko nitakakoketi niwahukumu mataifa yote yaliyo pande zote.
13 Haya! Utieni mundu, maana mavuno yameiva; njoni, kanyageni; kwa maana shinikizo limejaa, mapipa nayo yanafurika; kwani uovu wao ni mwingi sana.
14 Makutano makubwa, makutano makubwa, wamo katika bonde la kukata maneno! Kwa maana siku ya Bwana i karibu, katika bonde la kukata maneno.
15 Jua na mwezi vimetiwa giza, na nyota zimeacha kuangaza.
16 Naye Bwana atanguruma toka Sayuni, atatoa sauti yake toka Yerusalemu; na mbingu na nchi zitatetemeka; lakini Bwana atakuwa kimbilio la watu wake, na ngome ya wana wa Israeli.
17 Hivyo ndivyo mtakavyojua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, nikaaye Sayuni, mlima wangu mtakatifu; ndipo Yerusalemu utakapokuwa mtakatifu, wala wageni hawatapita tena ndani yake kamwe.
18 Tena itakuwa siku ile, ya kwamba milima itadondoza divai tamu, na vilima vitatiririka maziwa, na vijito vyote vya Yuda vitatoa maji tele; na chemchemi itatokea katika nyumba ya Bwana, na kulinywesha bonde la Shitimu.
19 Misri itakuwa ukiwa, na Edomu itakuwa jangwa tupu, kwa sababu ya dhuluma waliowatenda wana wa Yuda; kwa sababu wamemwaga damu isiyo na hatia katika nchi yao.
20 Bali Yuda atadumu milele, na Yerusalemu tangu kizazi hata kizazi.
21 Nami nitaitakasa damu yao ambayo sijaitakasa; kwa maana Bwana ndiye akaaye Sayuni.