Ayubu 5
1 Haya, ita sasa; je! Yuko atakayekujibu? Nawe utamwelekea yupi katika hao watakatifu?
2 Kwani hasira humwua mtu mpumbavu, Nao wivu humwua mjinga.
3 Nimewaona wapumbavu wakishusha mizizi; Lakini mara niliyalaani maskani yake.
4 Watoto wake wako mbali na wokovu, Nao wamesongwa langoni, Wala hapana atakayewaponya.
5 Mavuno yake wale wenye njaa huyala, Na kuyatwaa hata kuyatoa miibani, Nao wenye kiu huzitwetea mali zao.
6 Kwani taabu haitoki mchangani, Wala mashaka hayachipuki katika nchi;
7 Lakini mwanadamu huzaliwa ili apate mashaka, Kama cheche za moto zirukavyo juu.
8 Lakini mimi ningemtafuta Mungu, Ningemwekea Mungu daawa yangu;
9 Yeye afanyaye mambo makuu, yasiyotambulikana; Mambo ya ajabu yasiyo na hesabu;
10 Yeye atoaye mvua inyeshe juu ya nchi, Na kuyapeleka maji mashambani;
11 Awainuaye juu hao walio chini; Na hao waombolezao hukuzwa wawe salama.
12 Yeye huyatangua mashauri ya wadanganyifu, Mikono yao isipate kuyatimiza makusudi yao.
13 Yeye huwanasa wenye hekima katika hila yao wenyewe; Na mashauri ya washupavu yaharibika kwa haraka.
14 Wao hupatwa na giza wakati wa mchana, Hupapasa mchana vilevile kama usiku.
15 Lakini yeye huokoa na upanga wa kinywa chao, Hata kumwokoa mhitaji na mkono wake aliye hodari.
16 Basi hivi huyo maskini ana matumaini, Na uovu hufumba kinywa chake.
17 Tazama, yu heri mtu yule Mungu amwadhibuye; Kwa hiyo usidharau kurudiwa na huyo Mwenyezi.
18 Kwani yeye huumiza, lakini tena huuguza; Yeye hutia jeraha, na mikono yake huponya.
19 Yeye atakuokoa na mateso sita; Naam, hata katika saba hapana uovu utakaokugusa.
20 Wakati wa njaa atakukomboa na mauti; Na vitani atakukomboa na nguvu za upanga.
21 Utafichwa na mapigo ya ulimi; Wala usiogope maangamizo yatakapokuja.
22 Wewe utayacheka maangamizo na njaa; Wala hutawaogopa wanyama wakali wa nchi.
23 Kwani utakuwa na mapatano na mawe ya bara; Nao wanyama wa bara watakuwa na amani kwako.
24 Nawe utajua ya kwamba hema yako ina salama; Na zizi lako utaliaua, wala usikose kitu.
25 Tena utajua ya kwamba uzao wako utakuwa mwingi, Na vizazi vyako watakuwa kama nyasi za nchi.
26 Utafika kaburini mwenye umri mtimilifu, Kama mganda wa ngano ulivyo wakati wake.
27 Tazama, haya tumeyapeleleza, ndivyo yalivyo; Yasikie, uyajue, ili upate mema.