Ayubu 24
1 Mbona nyakati zisiwekwe na Mwenyezi? Na hao wamjuao mbona hawazioni siku zake?
2 Wako waziondoao alama za mipaka; Huyachukua makundi kwa jeuri na kuyalisha.
3 Humfukuza punda wake asiye baba, Humtwaa rehani ng'ombe wake mwanamke mjane.
4 Humgeuza mhitaji aiache njia; Maskini wa nchi hujificha pamoja.
5 Tazama, kama punda-mwitu jangwani Wao hutoka kwenda kazini mwao, wakitafuta chakula kwa bidii; Jangwa huwapa chakula cha watoto wao.
6 Hukata nafaka zao mashambani; Na kuokota zabibu za waovu.
7 Hujilaza usiku kucha uchi pasipo nguo, Wala hawana cha kujifunika baridi.
8 Hutota kwa manyunyo ya milimani, Na kuambatana na jabali kwa kukosa sitara,
9 Wako wamwondoao matitini kwa nguvu huyo asiye na baba, Na kutwaa rehani kwa maskini;
10 Hata wazunguke uchi pasipo mavazi, Nao wakiwa na njaa huchukua miganda;
11 Hushindika mafuta ndani ya makuta ya watu hao; Wakanyaga mashinikizo, nao wana kiu.
12 Watu huugua toka mji ulio na watu wengi, Na roho yake aliyejeruhiwa hupiga ukelele; Wala Mungu hauangalii upumbavu.
13 Hawa ni katika hao waliouasi mwanga; Hawazijui njia zake, Wala hawakai katika mapito yake.
14 Mwuaji huamka asubuhi kukipambauka, huwaua maskini na wahitaji; Tena wakati wa usiku yu kama mwivi.
15 Tena jicho lake mzinifu hungojea wakati wa giza-giza, Akisema, Hapana jicho litakaloniona; Naye huuficha uso wake.
16 Wao hutoboa nyumba gizani; Hujifungia ndani wakati wa mchana; Hawaujui mwanga.
17 Kwani asubuhi kwao wote ni kama giza tupu; Kwani wao wavijua vitisho vya hiyo giza tupu.
18 Mwasema, Yeye ni mwepesi juu ya uso wa gharika; Sehemu yao inalaaniwa duniani; Hageuki kwenda njia ya mizabibuni.
19 Chaka na hari hukausha maji ya theluji; Kuzimu nako hao ambao wamefanya dhambi.
20 Tumbo lililomzaa litamsahau; buu litamla na kuona tamu; Hatakumbukwa tena; Na udhalimu utavunjwa kama mti.
21 Naam, yeye huwala walio tasa wasiozaa; Wala hamtendei mema mwanamke mjane.
22 Lakini Mungu huwadumisha wenye uwezo kwa nguvu zake; Huinuka, wasiokuwa na tumaini la kuishi.
23 Huwapa kuwa na salama, nao wapumzika kwayo; Na macho yake ya juu ya njia zao.
24 Wao wametukuzwa; lakini kitambo kidogo hutoweka; Naam, hushushwa, na kuondolewa njiani kama wengine wote, Nao hukatwa kama vile masuke ya ngano.
25 Na kama sivyo sasa, ni nani atakayenihukumu kuwa ni mwongo, Na kuyafanya maneno yangu kuwa si kitu?