«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Ayubu 19

1  Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,

2  Je! Mtanichukiza nafsi yangu hata lini, Na kunivunja-vunja kwa maneno?

3  Mara kumi hizi mmenishutumu; Hamwoni haya kunifanyia mambo magumu.

4  Ingawaje nimekosa, Kosa langu hukaa kwangu mwenyewe.

5  Kwamba mtajitukuza juu yangu, Na kunena juu yangu shutumu langu;

6  Jueni basi kuwa Mungu amenipotosha, Na kunizingira kwa wavu wake.

7  Tazama, nalia, Udhalimu, lakini sisikiwi; Naulilia msaada, wala hapana hukumu.

8  Yeye ameiziba njia yangu nisipate kupita, Na kutia giza katika mapito yangu.

9  Amenivua utukufu wangu, Na kuiondoa taji kichwani mwangu.

10  Amenibomoa pande zote, nami nimetoweka; Na tumaini langu ameling'oa kama mti.

11  Tena ameziwasha ghadhabu zake juu yangu, Akanihesabia kuwa mmoja katika watesi wake.

12  Majeshi yake husongea pamoja, na kunipandishia njia yao, Na kupiga marago kuizunguka hema yangu.

13  Amewaweka ndugu zangu mbali nami, Na wanijuao wametengwa nami kabisa.

14  Watu wa mbari yangu wamekoma, Na rafiki zangu niwapendao wamenisahau.

15  Wakaao nyumbani mwangu, na vijakazi vyangu, wanihesabu kuwa mgeni; Mimi ni mgeni machoni pao.

16  Namwita mtumishi wangu, wala haniitikii, Ingawa namsihi kwa kinywa changu.

17  Pumzi zangu ni kama za mgeni kwa mke wangu, Nami ni machukizo kwa ndugu zangu.

18  Hata watoto wadogo hunidharau; Nikiondoka, huninena.

19  Wasiri wangu wote wanichukia; Na hao niliowapenda wamenigeukia.

20  Mfupa wangu unagandamana na ngozi yangu na nyama yangu, Nami nimeokoka na ngozi ya meno yangu tu.

21  Nihurumieni, nihurumieni, enyi rafiki zangu, Kwa maana mkono wa Mungu umenigusa.

22  Mbona ninyi mnaniudhi kama Mungu, Wala hamkutosheka na nyama yangu?

23  Laiti maneno yangu yangeandikwa sasa! Laiti yangeandikwa kitabuni!

24  Yakachorwa katika mwamba milele, Kwa kalamu ya chuma na risasi.

25  Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.

26  Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, Lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu;

27  Nami nitamwona mimi nafsi yangu, Na macho yangu yatamtazama, wala si mwingine.

28  Kama mkisema, Jinsi tutakavyomwudhi! Kwa kuwa shina la jambo hili limeonekana kwake;

29  Uogopeni upanga; Kwa maana adhabu za upanga zina ghadhabu, Mpate kujua ya kwamba hukumu iko.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23