Ayubu 18
1 Ndipo Bildadi, Mshuhi, akajibu, na kusema,
2 Je! Hata lini utayategea maneno mitambo? Fikiri, kisha baadaye tutanena.
3 Twahesabiwa kuwa wanyama kwa sababu gani, Tena kuwa wanajisi machoni pako?
4 Wewe ujiraruaye mwenyewe katika hasira yako, Je! Dunia itaachwa kwa ajili yako wewe? Au jabali litaondolewa mahali pake?
5 Naam, mwanga wa waovu utazimika, Wala mwali wa moto wake hautang'aa.
6 Mwanga hemani mwake utakuwa giza, Nayo taa iliyo juu yake itazimishwa.
7 Hatua zake za nguvu zitasongwa, Na shauri lake mwenyewe litamwangusha chini.
8 Kwani ametupwa katika wavu na miguu yake mwenyewe, Naye huenda juu ya matanzi.
9 Tanzi litamshika kisigino chake, Na mtambo utamgwia.
10 Amefichiwa tanzi chini, Na mtego amewekewa njiani.
11 Matisho yatamtia hofu pande zote, Na kumfukuza karibu na visigino vyake.
12 Nguvu zake zitaliwa na njaa, Na msiba utakuwa tayari kwa kusita kwake.
13 Utakula via vya mwili wake, Naam, mzaliwa wa kwanza wa mauti atavila via vyake.
14 Atang'olewa katika hema yake aliyokuwa akiitumaini; Naye atapelekwa kwake mfalme wa utisho.
15 Ambacho si chake kitakaa katika hema yake; Kiberiti kitamwagwa juu ya makazi yake.
16 Chini, mizizi yake itakaushwa; Na juu, tawi lake litasinyaa.
17 Kumbukumbu lake litakoma katika nchi, Wala hatakuwa na jina mashambani.
18 Atakimbizwa kutoka mwangani hata gizani, Na kufukuzwa atoke duniani.
19 Hatakuwa na mwana wala mjukuu kati ya watu wake, Wala hatasalia mtu hapo alipokaa.
20 Hao wanaokaa magharibi watastaajabia siku yake, Kama vile wanaokaa mashariki walivyotiwa hofu.
21 Hakika ndivyo yalivyo makazi ya wapotovu, Na hapa ni mahali pake asiyemjua Mungu.