Ayubu 17
1 Roho yangu imezimika, siku zangu zimekoma, Kaburi i tayari kunipokea.
2 Ni kweli wako kwangu wenye kufanya dhihaka, Jicho langu hukaa katika kunifanyia uchungu kwao.
3 Nipe rehani basi, uwe dhamana kwa ajili yangu kwako wewe mwenyewe; Kuna nani atakayeniwekea dhamana?
4 Kwani mioyo yao imeificha ufahamu; Kwa hiyo hutawakuza.
5 Awafitiniye rafiki zake wawe mawindo, Hata macho ya watoto wake yataingia kiwi.
6 Amenifanya niwe simo kwa watu; Nimekuwa mwenye kuchukiwa kwa wazi.
7 Jicho langu nalo limekuwa giza kwa sababu ya majonzi, Na via vyangu vyote vimekuwa kama kivuli.
8 Walekevu watayastaajabia hayo, Na asiye na hatia atajiamsha juu ya mpotovu.
9 Lakini mwenye haki ataishika njia yake, Naye mwenye mikono safi atazidi kupata nguvu.
10 Lakini rudini; ninyi nyote, njoni sasa; Wala sitampata mtu mwenye hekima kati yenu.
11 Siku zangu zimepita, makusudi yangu yamevunjika, Hata hayo niliyo nayo moyoni mwangu.
12 Wabadili usiku kuwa mchana; Wasema, Mwanga u karibu kwa sababu ya giza.
13 Nikitazamia kuzimu kuwa nyumba yangu; Nikitandika malazi yangu gizani;
14 Ikiwa nimeuita uharibifu, Wewe u baba yangu; Na kuliambia buu, Wewe u mama yangu, na umbu langu;
15 Basi, tumaini langu li wapi? Na tumaini langu, ni nani atakayeliona?
16 Litashuka kwenye makomeo ya kuzimu, Itakapokuwapo raha mavumbini.