Ayubu 15
1 Ndipo Elifazi, Mtemani, akajibu, na kusema,
2 Je! Yapasa mtu mwenye hekima kujibu kwa ujuzi wa uvuvio, Na kujaza tumbo lake na upepo wa mashariki?
3 Je! Ahoji na mazungumzo yasiyo faida, Au kwa maneno ambayo hawezi kufanya mema kwayo?
4 Naam, wewe waondoa kicho, Nawe wazuia ibada mbele za Mungu.
5 Kwani uovu wako unakufundisha kinywa chako, Nawe wachagua ulimi wake mwenye hila.
6 Kinywa chako mwenyewe chakuhukumia makosa, wala si mimi; Naam, midomo yako mwenyewe hushuhudia juu yako.
7 Je! Wewe u mtu wa kwanza aliyezaliwa? Au, ulizawa wewe kabla ya milima?
8 Je! Umesikia mashauri ya siri ya Mungu? Nawe je! Wazuia hekima iwe yako tu?
9 Je! Wewe wajua neno lipi, ambalo sisi hatulijui? Nawe wafahamu nini, ambalo halimo ndani yetu?
10 Wenye mvi, na walio wazee sana, wote wapo pamoja nasi, Ambao ni wazee kuliko baba yako.
11 Je! Utulizi wa Mungu ni mdogo sana kwako, Na hilo neno la upole si kitu kwako?
12 Mbona moyo wako unakutaharakisha! Na macho yako, je! Kwani kung'ariza?
13 Hata ukageuza roho yako iwe kinyume cha Mungu, Na kuyatoa maneno kama hayo kinywani mwako.
14 Je! Mwanadamu ni kitu gani, hata akawa safi? Huyo aliyezaliwa na mwanamke, hata awe na haki?
15 Yeye hawategemei watakatifu wake; Naam, mbingu nazo si safi machoni pake.
16 Sembuse mtu ambaye ni mwenye kuchukiza na uchafu, Mwanadamu anywaye uovu kama anywavyo maji!
17 Mimi nitakuonyesha, unisikilize; Na hayo yote niliyoyaona nitayanena;
18 (Ambayo watu wenye hekima wameyatangaza Tokea baba zao, wala hawakuyaficha;
19 Waliopewa hiyo nchi peke yao, Wala mgeni hakupita kati yao);
20 Mtu mwovu huwa na uchungu siku zake zote, Hata hesabu ya miaka aliyowekewa mwenye kuonea.
21 Sauti za utisho zi masikioni mwake; Katika kufanikiwa kwake mtekaji nyara atamjia juu yake;
22 Yeye hasadiki kwamba atarudi kutoka gizani, Naye hungojewa na upanga;
23 Hutanga-tanga ili apate chakula, akisema, Ki wapi? Ajua kwamba siku ya giza i tayari karibu yake;
24 Mateso na dhiki humtia hofu; Humshinda kama vile mfalme aliye tayari kwa vita;
25 Kwa kuwa amenyosha mkono wake juu ya Mungu, Na kuendelea kwa kiburi kinyume cha Mwenyezi;
26 Humshambulia na shingo ngumu, Kwa mafundo makubwa ya ngao zake;
27 Kwa kuwa amefunika uso wake na kunona kwake, Na kuwandisha mafuta kiunoni mwake; Naye amekaa katika miji iliyo ukiwa,
28 Katika nyumba ambazo hapana mtu azikaaye, Zilizokuwa tayari kuwa magofu.
29 Hatakuwa tajiri, wala mali zake hazitadumu, Wala maongeo yao hayatainama nchi.
30 Hataondoka gizani; Ndimi za moto zitayakausha matawi yake, Naye ataondoka kwa pumzi za kinywa chake.
31 Asiutumainie ubatili, na kujidanganya; Kwa kuwa huo ubatili ndio utakaokuwa ujira wake.
32 Jambo hili litatendeka kabla ya wakati wake, Na tawi lake halitasitawi.
33 Atayapukutisha mapooza yake kama mzabibu, Na kuyatupa maua yake kama mzeituni.
34 Kwa kuwa jamii ya hao wasiomcha Mungu watakuwa tasa, Na moto utateketeza mahema yenye rushwa.
35 Wao hutunga mimba ya madhara, na kuzaa uovu, Nalo tumbo lao hutengeza udanganyifu.