Ayubu 14
1 Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu.
2 Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa; Hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe.
3 Nawe, je! Wafumbua macho yako kumwangalia mtu kama yeye, Na kunitia katika hukumu pamoja nawe?
4 Ni nani awezaye kutoa kitu kilicho safi kitoke katika kitu kichafu? Hapana awezaye.
5 Kwa kuwa siku zake zimeamriwa, hesabu ya miezi yake unayo wewe, Nawe umemwekea mipaka yake asiyoweza kuipita;
6 Acha kumwangalia yeye, apate kupumzika, Hata atakapoitimiza siku yake, kama aliyeajiriwa.
7 Kwani yako matumaini ya mti, ya kuwa ukikatwa utachipuka tena, Wala machipukizi yake hayatakoma.
8 Ijapokuwa mizizi yake huchakaa mchangani, Na shina lake kufa katika udongo;
9 Lakini kwa harufu ya maji utachipuka, Na kutoa matawi kama mche.
10 Lakini mwanadamu hufa, huifariki dunia; Naam, mwanadamu hutoa roho, naye yupo wapi?
11 Kama vile maji kupwa katika bahari, Na mto kupunguka na kukatika;
12 Ni vivyo mwanadamu hulala chini, asiinuke; Hata wakati wa mbingu kutokuwako tena, hawataamka, Wala kuamshwa usingizini.
13 Laiti ungenificha kuzimuni, Ukanilinda kwa siri, hata ghadhabu zako zitakapopita, Na kuniandikia muda ulioamriwa, na kunikumbuka!
14 Mtu akifa, je! Atakuwa hai tena? Mimi ningengoja siku zote za vita vyangu, Hata kufunguliwa kwangu kunifikilie.
15 Wewe ungeita, nami ningekujibu; Ungekuwa na tamaa ya kazi ya mikono yako.
16 Lakini sasa wazihesabu hatua zangu; Je! Huchungulii dhambi yangu?
17 Kosa langu limetiwa muhuri mfukoni, Nawe waufunga uovu wangu.
18 Lakini, tazama, mlima ukianguka hutoweka, Nalo jabali huondolewa mahali pake;
19 Maji mengi huyapunguza mawe; Mafuriko yake huuchukua mchanga wa nchi; Nawe matumaini ya wanadamu wayaangamiza.
20 Wewe wamshinda nguvu sikuzote, naye hupita aende zake Wabadili sura zake, na kumpeleka aondoke.
21 Wanawe hufikilia heshima, wala yeye hajui; Kisha wao huaibishwa, lakini yeye hana habari zao.
22 Lakini mwili ulio juu yake una maumivu, Na nafsi yake ndani huomboleza.