«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Ayubu 1

1  Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu.

2  Kisha walizaliwa kwake wana saba, na binti watatu.

3  Mali yake nayo yalikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng'ombe mia tano, na punda wake mia tano, na watu wa nyumbani wengi sana; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki.

4  Nao wanawe huenda na kufanya karamu katika nyumba ya kila mmoja wao kwa siku yake; nao wakatuma na kuwaita maumbu yao watatu ili waje kula na kunywa pamoja nao.

5  Basi ilikuwa, hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia, Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani Ayubu alisema, Yumkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi, na kumkufuru Mungu mioyoni mwao. Ndivyo alivyofanya Ayubu sikuzote.

6  Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao.

7  Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo.

8  Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu.

9  Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure?

10  Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi.

11  Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.

12  Bwana akamwambia Shetani, Tazama, yote aliyo nayo yamo katika uwezo wako; lakini usinyoshe mkono wako juu yake yeye mwenyewe. Basi Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana.

13  Ilitukia siku moja hao wanawe na binti zake walipokuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa,

14  mjumbe akamfikilia Ayubu na kumwambia, Hao ng'ombe walikuwa wakilima, na punda walikuwa wakilisha karibu nao;

15  mara Waseba wakawashambulia, wakawachukua wakaenda nao; naam, wamewaua hao watumishi kwa makali ya upanga, mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.

16  Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Moto wa Mungu umeanguka kutoka mbinguni na kuwateketeza kondoo, na wale watumishi, na kuwaangamiza; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.

17  Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wakaldayo walifanya vikosi vitatu, wakawaangukia ngamia, wakaenda nao, naam, wamewaua wale watumishi kwa makali ya upanga; mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.

18  Huyo alipokuwa akali akinena, akatokea na mwingine, na kusema, Wanao na binti zako walikuwa wakila na kunywa divai katika nyumba ya ndugu yao mkubwa;

19  mara, tazama, upepo wenye nguvu ukatoka pande za jangwani, ukaipiga hiyo nyumba pembe zake nne, nayo ikawaangukia hao vijana, nao wamekufa; na mimi peke yangu nimepona, mimi tu, kukuletea habari.

20  Ndipo Ayubu akainuka, akalirarua joho lake, kisha akanyoa kichwa chake, na kuanguka chini, na kusujudia;

21  akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe.

22  Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23