Yeremia 9
1 Laiti kichwa changu kingekuwa maji, na macho yangu kuwa chemchemi ya machozi, ili nipate kulia mchana na usiku kwa ajili yao waliouawa wa binti ya watu wangu!
2 Laiti ningekuwa na mahali pa kukaa jangwani, kibanda cha wasafiri; nipate kuwaacha watu wangu, na kuondoka kwao! Maana wao ni wazinzi, wote pia, mkutano wa watu wenye hiana.
3 Huupinda ulimi wao, kana kwamba ni upinde, ili kusema uongo; nao wamepata nguvu katika nchi, lakini si katika uaminifu; maana huendelea toka ubaya hata ubaya, wala hawanijui mimi, asema Bwana.
4 Jihadharini, kila mtu na jirani yake, wala msimtumaini ndugu awaye yote; maana kila ndugu atachongea, na kila jirani atakwenda huko na huko na kusingizia.
5 Nao watadanganya kila mtu jirani yake, wala hawatasema kweli; wameuzoeza ulimi wao kusema uongo; hujidhoofisha ili kutenda uovu.
6 Makao yako ya katikati ya hadaa; kwa hadaa wanakataa kunijua mimi, asema Bwana.
7 Basi, kwa hiyo Bwana wa majeshi asema hivi, Tazama, nitawayeyusha na kuwajaribu; maana nisipotenda hivi, nitende nini kwa ajili ya binti ya watu wangu?
8 Ulimi wao ni mshale ufishao; husema maneno ya hadaa; mtu mmoja husema maneno ya amani na mwenzake kwa kinywa chake, lakini moyoni mwake humwotea.
9 Je! Nisiwapatilize kwa mambo hayo? Asema Bwana; na nafsi yangu je! Nisijilipize kisasi juu ya taifa la namna hii?
10 Kwa milima nitalia na kulalama, Na kwa malisho ya nyikani nitafanya maombolezo; Kwa sababu yameteketea, hata hapana apitaye, Wala hapana awezaye kusikia sauti ya ng'ombe; Ndege wa angani, na wanyama wa mwituni, Wamekimbia, wamekwenda zao.
11 Nami nitafanya Yerusalemu kuwa magofu, Makao ya mbweha; Nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa, Isikaliwe na mtu awaye yote.
12 Ni nani aliye na hekima, apate kuelewa na haya? Tena ni nani ambaye kinywa cha Bwana kimesema naye, apate kuyatangaza? Nayo ni nini maana yake nchi hii kuharibika, na kuteketea kama nyika, asipite mtu?
13 Naye Bwana asema, Ni kwa sababu wameiacha sheria yangu niliyoweka mbele yao, wala hawakuitii sauti yangu, wala kuenenda katika hiyo;
14 bali wameenenda katika ushupavu wa mioyo yao wenyewe, na kuandamana na Mabaali, kama walivyofundishwa na baba zao.
15 Basi, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitawalisha pakanga, naam, watu hawa, nami nitawapa maji ya uchungu wayanywe.
16 Nami nitawatawanya kati ya mataifa, ambao wao hawakuwajua; wala baba zao, nami nitatuma upanga nyuma yao, hata nitakapowaangamiza kabisa.
17 Bwana wa majeshi asema hivi, Fikirini ninyi, mkawaite wanawake waombolezao, ili waje; mkatume na kuwaita wanawake wenye ustadi, ili waje;
18 na wafanye haraka na kutuombolezea, ili macho yetu yachuruzike machozi, na kope zetu zibubujike maji.
19 Maana sauti ya maombolezo imesikiwa toka Sayuni, Jinsi tulivyotekwa! tulivyofadhaika sana! Kwa sababu tumeiacha nchi, kwa kuwa wameangusha makao yetu.
20 Lakini lisikieni neno la Bwana, enyi wanawake, Na masikio yenu yapokee neno la kinywa chake; Mkawafundishe binti zenu kuomboleza, Na kila mmoja jirani yake kulia.
21 Kwa maana mauti imepandia madirishani mwetu, imeingia majumbani mwetu; Ipate kuwakatilia mbali watoto walio nje, na vijana katika njia kuu.
22 Nena, Bwana asema hivi, Mizoga ya watu itaanguka kama samadi juu ya mashamba, Na kama konzi ya ngano nyuma yake avunaye, wala hapana mtu atakayeikusanya.
23 Bwana asema hivi, Mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya hekima yake, wala mwenye nguvu asijisifu kwa sababu ya nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa sababu ya utajiri wake;
24 bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitendaye wema, na hukumu, na haki, katika nchi; maana mimi napendezwa na mambo hayo, asema Bwana,
25 Tazama, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapowaadhibu wote waliotahiriwa katika hali yao ya kutokutahiriwa;
26 Misri, na Yuda, na Edomu, na wana wa Amoni, na Moabu, na wote wenye kunyoa denge, wakaao nyikani; maana mataifa hayo yote hawana tohara, wala nyumba yote ya Israeli hawakutahiriwa mioyo yao.