Yeremia 48
1 Habari za Moabu. Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Ole wake Nebo! Kwa maana umeharibika; Kiriathaimu umeaibishwa, umetwaliwa; Misgabu umeaibishwa, nao umebomolewa.
2 Sifa za Moabu haziko tena; katika Heshboni wameazimia mabaya juu yake, Haya! Njoni, na tumkatilie mbali asiwe taifa. Wewe nawe, Ee Madmena, utanyamazishwa; upanga utakufuatia.
3 Sauti ya kilio toka Horonaimu, Ya kutekwa na uharibifu mkuu.
4 Moabu umeharibika; Wadogo wake wamewasikiza watu kilio.
5 Kwa maana watu wapandapo huko Luhithi Watapanda wasiache kulia; Nao watu watelemkapo huko Horonaimu Wameisikia huzuni ya kilio cha uharibifu.
6 Haya! Kimbieni! Jiokoeni nafsi zenu! Mkawe kama mtu aliye mkiwa.
7 Maana, kwa kuwa umeyatumainia matendo yako, na hazina zako, wewe nawe utatwaliwa; na Kemoshi atatoka aende katika uhamisho, makuhani wake na wakuu wake pamoja.
8 Naye mwenye kuteka nyara atakuja juu ya kila mji, wala hapana mji utakaookoka; bonde nalo litaangamia, nayo nchi tambarare itaharibiwa; kama Bwana alivyosema.
9 Mpe Moabu mabawa, apate kuruka na kwenda zake; na miji yake itakuwa ukiwa, isiwe na mtu wa kukaa ndani yake.
10 Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya Bwana kwa ulegevu; na alaaniwe auzuiaye upanga wake usimwage damu.
11 Moabu amestarehe tangu ujana wake, naye ametulia juu ya sira zake, wala hakumiminwa kutoka chombo kimoja kutiwa chombo kingine, wala hakwenda kufungwa; kwa hiyo ladha yake anakaa nayo, wala harufu yake haikubadilika.
12 Basi, tazama, siku zinakuja, asema Bwana, ambazo nitampelekea wamiminao, nao watammimina, nao watamwaga vyote vilivyomo vyomboni mwake, na kuzivunja chupa zake vipande vipande.
13 Na Moabu ataona haya kwa ajili ya Kemoshi, kama nyumba ya Israeli ilivyoona haya kwa ajili ya Betheli, matumaini yao.
14 Mwasemaje ninyi, Sisi tu mashujaa, watu hodari wa vita.
15 Moabu ameharibika, na moshi wa miji yake umepanda; na vijana wake wateule wametelemka kwenda kuchinjwa, asema Mfalme, ambaye jina lake ni Bwana wa majeshi.
16 Msiba wa Moabu umefika karibu, Na mateso yake yanafanya haraka.
17 Ninyi nyote mnaomzunguka, mlilieni, Nanyi nyote mlijuao jina lake, semeni, Jinsi ilivyovunjika fimbo ya enzi, Fimbo ile iliyokuwa nzuri!
18 Ee binti ukaaye Diboni, Shuka toka utukufu wako, ukae katika kiu; Maana atekaye Moabu amepanda juu yako, Ameziharibu ngome zako.
19 Wewe ukaaye Aroeri, Simama kando ya njia upeleleze; Mwulize mwanamume akimbiaye na mwanamke atorokaye, Sema, Imetendeka nini?
20 Moabu ameaibishwa, kwa maana amevunjika; Pigeni yowe na kulia; Tangazeni habari hii katika Arnoni, Ya kuwa Moabu ameharibika.
21 Na hukumu imeifikilia nchi tambarare; juu ya Holoni, na juu ya Yasa, na juu ya Mefaathi;
22 na juu ya Diboni, na juu ya Nebo, na juu ya Beth-diblathaimu;
23 na juu ya Kiriathaimu, na juu ya Beth-gamuli, na juu ya Beth-meoni;
24 na juu ya Keriothi, na juu ya Bozra, na juu ya miji yote ya nchi ya Moabu, iliyo mbali na iliyo karibu.
25 Pembe ya Moabu imekatika, na mkono wake umevunjika, asema Bwana. Mlevyeni; kwa maana alijitukuza juu ya Bwana
26 na Moabu atagaa-gaa katika matapiko yake, naye atadhihakiwa. Kwa maana Israeli, je! Hakuwa dhihaka kwako?
27 Alionekana kati ya wevi? Maana kila umtajapo watikisa kichwa chako.
28 Enyi mkaao Moabu, iacheni miji, Enendeni kukaa majabalini; Mkawe kama njiwa afanyaye kioto chake Katika ubavu wa mdomo wa shimo.
29 Tumesikia habari za kiburi cha Moabu; Ya kuwa ana kiburi kingi; Jeuri yake, na kiburi chake, na majivuno yake, Na jinsi alivyotakabari moyoni mwake.
30 Najua ghadhabu yake, asema Bwana, ya kuwa si kitu; majisifu yake hayakutenda neno lo lote.
31 Kwa sababu hiyo nitampigia yowe Moabu, naam, nitapiga kelele kwa ajili ya Moabu yote; nitawaombolezea watu wa Kir-heresi.
32 Nitakulilia, Ee mzabibu wa Sibma, kwa vilio vipitavyo vilio vya Yazeri; matawi yako yalipita juu ya bahari, yalifika hata bahari ya Yazeri; atekaye nyara ameyaangukia matunda yako ya wakati wa jua, na mavuno yako ya zabibu.
33 Furaha na shangwe zimeondoshwa, katika shamba lizaalo sana, na katika nchi ya Moabu; nami nimeikomesha divai katika mashinikizo; hapana mtu atakayekanyaga zabibu kwa shangwe; shangwe ile itakuwa si shangwe.
34 Toka kilio cha Heshboni mpaka Eleale, naam, mpaka Yahasa, wametoa sauti zao, toka Soari mpaka Horonaimu, hata Eglath-shelishia; maana maji ya Nimrimu nayo yatakuwa ukiwa.
35 Pamoja na hayo, asema Bwana, nitamkomesha katika Moabu mtu atoaye sadaka katika mahali pa juu, naye awafukiziaye uvumba miungu yake.
36 Kwa sababu hiyo moyo wangu watoa sauti kama filimbi kwa ajili ya Moabu, na kwa ajili ya watu wa Kir-heresi, moyo wangu watoa sauti kama filimbi; kwa kuwa wingi aliojipatia umepotea.
37 Maana kila kichwa kina upaa, na ndevu zote zimenyolewa; mikono yote ina alama za chale, na viuno vyote vimevikwa nguo za magunia.
38 Juu ya dari zote za nyumba za Moabu, na katika njia kuu zake, pana maombolezo, kila mahali; kwa maana nimevunja Moabu kama chombo kisichopendeza, asema Bwana.
39 Jinsi alivyovunjika! Pigeni yowe! Jinsi Moabu alivyogeuza kisogo kwa haya! Hivyo ndivyo Moabu atakavyokuwa dhihaka, na sababu ya kuwashangaza watu wote wamzungukao.
40 Maana Bwana asema hivi, Tazama, ataruka kama tai, na kutandaza mabawa yake juu ya Moabu.
41 Miji imetwaliwa, ngome zimeshambuliwa, na mioyo ya mashujaa wa Moabu siku hiyo itakuwa kama moyo wa mwanamke katika utungu wake.
42 Na Moabu ataangamizwa, asiwe taifa tena, kwa sababu alijitukuza juu ya Bwana.
43 Hofu, na shimo, na mtego, zaja juu yako, Ee mwenyeji wa Moabu, asema Bwana.
44 Aikimbiaye hofu ataanguka shimoni; na yeye atokaye shimoni atanaswa kwa mtego; maana nitaleta juu yake, yaani, juu ya Moabu, mwaka wa kujiliwa kwake, asema Bwana.
45 Wamekimbia, wasio na nguvu Wanasimama chini ya kivuli cha Heshboni; Ila moto umetoka katika Heshboni, Na mwali wa moto toka kati ya Sihoni Nao umekula pembe ya Moabu, Na utosi wa kichwa wa watu wapigao kelele.
46 Ole wako! Ee Moabu, Watu wa Kemoshi wamepotea; Maana wana wako wamechukuliwa mateka, Na binti zako wamekwenda utumwani.
47 Lakini nitawarudisha watu wa Moabu walio utumwani, siku za mwisho, asema Bwana. Hukumu ya Moabu imefikilia hapa.