Yeremia 39
1 Hata ikawa, Yerusalemu ulipotwaliwa, (katika mwaka wa kenda wa Sedekia, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa kumi, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, na jeshi lake lote, wakaja juu ya Yerusalemu, wakauhusuru;
2 katika mwaka wa kumi na mmoja wa Sedekia, mwezi wa nne, siku ya kenda ya mwezi, sehemu ya ukuta wa mji ilibomolewa;)
3 wakuu wote wa mfalme wa Babeli wakaingia, wakaketi katika lango la katikati, yaani, Nergal-Shareza, mnyweshaji, Nebu-Sarseki, mkuu wa matowashi, Nergal-Shareza, mkuu wa wanajimu,
4 Ikawa Sedekia, mfalme wa Yuda, na watu wote wa vita walipowaona, ndipo wakakimbia, wakatoka mjini usiku, kwa njia ya bustani ya mfalme, kwa lango lililokuwa kati ya zile kuta mbili; naye akatoka kwa njia ya Araba.
5 Lakini jeshi la Wakaldayo wakawafuatia, wakampata Sedekia katika nchi tambarare ya Yeriko; nao walipomkamata, wakamleta kwa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, huko Ribla katika nchi ya Hamathi, naye akatoa hukumu juu yake.
6 Ndipo mfalme wa Babeli akawaua wana wa Sedekia huko Ribla mbele ya macho yake; pia mfalme wa Babeli akawaua wakuu wote wa Yuda.
7 Pamoja na hayo akampofusha macho Sedekia, akamfunga kwa pingu ili amchukue mpaka Babeli.
8 Nao Wakaldayo wakaiteketeza nyumba ya mfalme, na nyumba za watu kwa moto, wakazibomoa kuta za Yerusalemu.
9 Basi, Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawachukua mateka mabaki ya watu waliosalia katika mji mpaka Babeli, na hao pia waliouacha mji na kujiunga naye, na mabaki ya watu waliosalia.
10 Lakini Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawaacha baadhi ya maskini wa watu, waliokuwa hawana kitu, katika nchi ya Yuda, akawapa mashamba ya mizabibu na makonde wakati uo huo.
11 Basi Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akamwagiza Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, katika habari za Yeremia, akisema,
12 Mtwae, umtunze sana, wala usimtende neno baya lo lote; lakini umtendee kama atakavyokuambia.
13 Basi Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, na Nebu-Shazbani, mkuu wa matowashi, na Nergal-Shareza, mkuu wa wanajimu,
14 wakatuma watu wakamwondoa Yeremia katika uwanda wa walinzi, wakamweka katika mikono ya Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, ili ampeleke nyumbani kwake; basi akakaa pamoja na hao watu.
15 Basi neno la Bwana likamjia Yeremia, wakati ule alipokuwa amefungwa katika uwanda wa walinzi, kusema,
16 Haya! Enenda ukaseme na Ebedmeleki, Mkushi, kusema, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitaupatiliza mji huu maneno yangu kwa mabaya, wala si kwa mema; nayo yatatimizwa mbele yako katika siku hiyo.
17 Lakini nitakuokoa wewe katika siku hiyo, asema Bwana; wala hutatiwa katika mikono ya watu wale unaowaogopa.
18 Kwa maana ni yakini, nitakuokoa, wala hutaanguka kwa upanga, lakini nafsi yako itakuwa kama nyara kwako; kwa kuwa ulinitumaini mimi, asema Bwana.