Yeremia 25
1 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, katika habari za watu wote wa Yuda; katika mwaka wa nne wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda mwaka ule ndio mwaka wa kwanza wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli;
2 ambalo Yeremia, nabii, aliwaambia watu wote wa Yuda, na wenyeji wote wa Yerusalemu, kusema,
3 Tangu mwaka wa kumi na tatu wa kutawala kwake Yosia, mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda, hata siku hii ya leo, miaka hii ishirini na mitatu, neno la Bwana limenijia, nami nimesema nanyi, nikiamka mapema na kusema; lakini ninyi hamkusikiliza.
4 Naye Bwana ametuma kwenu watumishi wake wote, hao manabii, akiamka mapema na kuwatuma, lakini ninyi hamkusikiliza, wala hamkutega masikio yenu, msikilize.
5 Akasema, Rudini sasa, kila mtu na aiache njia yake mbaya; uacheni uovu wa matendo yenu, mkae katika nchi ambayo Bwana aliwapa, ninyi na baba zenu, tangu zamani za kale na hata milele;
6 wala msiwafuate miungu mingine, ili kuwatumikia na kuwasujudia, wala msinikasirishe kwa kazi ya mikono yenu; basi, mimi sitawadhuru ninyi kwa dhara lo lote.
7 Lakini ninyi hamkunisikiliza, asema Bwana; ili mnikasirishe kwa kazi ya mikono yenu, na kujidhuru nafsi zenu.
8 Basi Bwana wa majeshi asema hivi, Kwa kuwa hamkuyasikiliza maneno yangu,
9 angalieni, nitapeleka watu na kuzitwaa jamaa zote za upande wa kaskazini, asema Bwana, nami nitatuma ujumbe kwa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, mtumishi wangu, nami nitawaleta juu ya nchi hii, na juu yao wakaao ndani yake, na juu ya mataifa haya yote yaliyopo pande zote; nami nitawaangamiza kabisa, na kuwafanya kitu cha kushangaza, na kitu cha kuzomewa, na ukiwa wa daima.
10 Tena, nitawaondolea sauti ya kicheko, na sauti ya furaha, sauti ya bwana arusi, na sauti ya bibi arusi, sauti ya mawe ya kusagia, na nuru ya mishumaa.
11 Na nchi hii yote pia itakuwa ukiwa, na kitu cha kushangaza; nayo mataifa haya watamtumikia mfalme wa Babeli miaka sabini.
12 Na itakuwa miaka hiyo sabini itakapotimia, nitamwadhibu mfalme wa Babeli, na taifa lile, asema Bwana, kwa sababu ya uovu wao, nayo nchi ya Wakaldayo pia; nami nitaifanya kuwa ukiwa wa milele.
13 Nami nitaleta juu ya nchi ile maneno yangu yote niliyoyanena juu yake, naam, yote yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki, aliyotabiri Yeremia juu ya mataifa haya yote.
14 Kwa maana mataifa mengi na wafalme wakuu watawatumikisha; naam, hao pia; nami nitawalipa kwa kadiri ya matendo yao, na kwa kadiri ya kazi ya mikono yao.
15 Maana Bwana, Mungu wa Israeli, aniambia hivi, Pokea kikombe cha divai ya ghadhabu hii mkononi mwangu, ukawanyweshe mataifa yote, ambao nitakupeleka kwao;
16 nao watakunywa, na kulewalewa, na kufanya wazimu, kwa sababu ya upanga nitakaoupeleka kati yao.
17 Ndipo nikakipokea kikombe kile mkononi mwa Bwana, nikawanywesha mataifa yote, ambao Bwana alinipeleka kwao;
18 yaani, Yerusalemu, na miji ya Yuda, na wafalme wake, na wakuu wake, ili kuwafanya kuwa ukiwa, na ajabu, na mazomeo, na laana; vile vile kama ilivyo leo;
19 Farao, mfalme wa Misri, na watumishi wake na wakuu wake na watu wake wote;
20 na watu wote waliochanganyika pamoja, na wafalme wote wa nchi ya Uzi, na wafalme wote wa nchi ya Wafilisti, na Ashkeloni, na Gaza, na Ekroni, na mabaki ya Ashdodi;
21 Edomu, na Moabu, na wana wa Amoni;
22 na wafalme wote wa Tiro, na wafalme wote wa Sidoni, na wafalme wote wa kisiwa kilicho ng'ambo ya pili ya bahari;
23 Dedani, na Tema, na Buzi, na watu wote wakatao denge;
24 na wafalme wote wa Arabuni, na wafalme wote wa watu waliochanganyika wakaao jangwani;
25 na wafalme wote wa Zimri, na wafalme wote wa Elamu, na wafalme wote wa Wamedi;
26 na wafalme wote wa kaskazini, walio mbali na walio karibu, wote pamoja; na wafalme wote wa dunia, wakaao juu ya uso wa dunia; na mfalme wa Sheshaki
27 Nawe utawaambia hivi, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nyweni, na kulewa, na kutapika, na kuanguka msiinuke tena, kwa sababu ya upanga nitakaoupeleka kati yenu.
28 Tena itakuwa, kama wakikataa kukipokea kikombe kile mkononi mwako, wanywe, ndipo utakapowaambia, Bwana wa majeshi asema hivi, Lazima mtakunywa.
29 Maana angalieni, ninaanza kutenda mabaya katika mji uitwao kwa jina langu, je! Mtaachiliwa ninyi msiadhibiwe? Hamtaachiliwa msiadhibiwe; kwa maana nitauita upanga ule uwapige wote wakaao katika dunia, asema Bwana wa majeshi.
30 Basi, tabiri wewe maneno haya yote juu yao, na kuwaambia, Bwana atanguruma toka juu, Naye atatoa sauti yake toka patakatifu pake; Atanguruma sana juu ya zizi lake; Atapiga kelele kama mtu akanyagaye zabibu, Juu ya wenyeji wote wa dunia.
31 Mshindo utafika hata mwisho wa dunia; Maana Bwana ana mashindano na mataifa, Atateta na watu wote wenye mwili; Na waovu atawatoa wauawe kwa upanga; asema Bwana.
32 Bwana wa majeshi asema hivi, Tazama, uovu utatokea toka taifa hata taifa, na tufani kuu itainuliwa toka pande za mwisho wa dunia.
33 Na waliouawa na Bwana siku ile watakuwapo, toka upande mmoja wa dunia hata upande wa pili; hawataliliwa, wala kukusanywa, wala kuzikwa; watakuwa samadi juu ya uso wa nchi.
34 Pigeni yowe, enyi wachungaji, na kulia; na kugaagaa katika majivu, enyi mlio hodari katika kundi; maana siku za kuuawa kwenu zimetimia kabisa, nami nitawavunja vipande vipande, nanyi mtaanguka kama chombo cha anasa.
35 Nao wachungaji watakuwa hawana njia ya kukimbia, wala walio hodari katika kundi hawataokoka.
36 Sauti ya kilio cha wachungaji, na sauti ya kupiga yowe kwao walio hodari katika kundi, kwa maana Bwana anayaharibu malisho yao.
37 Na mazizi yenye amani yamenyamazishwa, kwa sababu ya hasira kali ya Bwana.
38 Ameacha mahali pake pa kujificha, kama simba; maana nchi yao imekuwa kitu cha kushangaza, kwa sababu ya ukali wa upanga uoneao, na kwa sababu ya hasira yake kali.