«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Isaya 64

1  Laiti ungepasua mbingu, na kushuka, ili milima iteteme mbele zako;

2  kama vile moto uchomapo vichaka, na moto uchemshapo maji; ili kuwajulisha adui zako jina lako, mataifa wakatetemeke mbele zako!

3  Ulipofanya mambo ya kutisha tusiyoyatazamia, ulishuka, milima ikatetema mbele zako.

4  Maana tangu zamani za kale watu hawakusikia, wala kufahamu kwa masikio, wala jicho halikuona Mungu, ila wewe, atendaye mambo kwa ajili yake amngojaye.

5  Wewe wamlaki yeye afurahiaye yaliyo haki na kuyatenda, watu wale wakukumbukao katika njia zako; tazama, ulikuwa na hasira, nasi tulitenda dhambi; tumekuwa katika mambo haya muda mwingi; nasi, je! Tutaokolewa?

6  Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi; sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo.

7  Tena hapana aliitiaye jina lako, ajitahidiye akushike; kwa kuwa umetuficha uso wako, nawe umetukomesha kwa njia ya maovu yetu.

8  Lakini sasa, Ee Bwana, wewe u baba yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu; sisi sote tu kazi ya mikono yako.

9  Ee Bwana, usione hasira nyingi, wala usiukumbuke uovu siku zote; tazama, angalia, twakusihi, sisi sote tu watu wako.

10  Miji yako mitakatifu imekuwa jangwa, Sayuni umekuwa jangwa, Yerusalemu umekuwa ukiwa.

11  Nyumba yetu takatifu, nzuri, walimokusifu baba zetu, imeteketea moto; vitu vyetu vyote vyenye kupendeza vimeharibika.

12  Utajizuia usiyaangalie mambo haya, Ee Bwana? Utanyamaza, na kututesa sana?

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23