«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Isaya 48

1  Sikieni haya, enyi watu wa nyumba ya Yakobo, mnaoitwa kwa jina la Israeli, mliotoka katika maji ya Yuda; mnaoapa kwa jina la Bwana, na kumtaja Mungu wa Israeli, lakini si kwa kweli, wala si kwa haki.

2  Maana hujiita wenyeji wa mji mtakatifu, hujitegemeza juu ya Mungu wa Israeli; Bwana wa majeshi ni jina lake.

3  Mimi nimehubiri mambo ya kale tangu zamani; naam, yalitoka katika kinywa changu, nikayadhihirisha; naliyatenda kwa ghafula, yakatokea.

4  Kwa sababu nalijua ya kuwa wewe u mkaidi, na shingo yako ni shingo ya chuma, na kipaji cha uso wako ni shaba;

5  basi nimekuonyesha tangu zamani; kabla hayajatukia nalikuonyesha; usije ukasema, Sanamu yangu imetenda haya; sanamu yangu ya kuchonga, na sanamu yangu ya kuyeyusha, imeyaamuru.

6  Umesikia haya; tazama haya yote; nanyi, je! Hamtayahubiri? Nimekuonyesha mambo mapya tangu wakati huu, naam, mambo yaliyofichwa, usiyoyajua.

7  Yameumbwa sasa, wala si tokea zamani; na kabla ya siku hii ya leo hukusikia habari yake; usije ukasema, Tazama, naliyajua.

8  Naam, hukusikia; naam, hukujua; naam, tokea zamani sikio lako halikuzibuka; maana nalijua ya kuwa wewe watenda kwa hila nyingi, nawe umeitwa mkosaji tangu kuzaliwa kwako;

9  kwa ajili ya jina langu nitaahirisha hasira yangu, na kwa ajili yako nitajizuia, ili nisifiwe, wala nisikukatilie mbali.

10  Tazama, nimekusafisha, lakini si kama fedha; nimekuchagua katika tanuru ya mateso.

11  Kwa ajili ya nafsi yangu, kwa ajili ya nafsi yangu, nitatenda haya; je! Litiwe unajisi jina langu? Wala sitampa mwingine utukufu wangu.

12  Nisikilize mimi, Ee Yakobo; na Israeli, niliyekuita; mimi ndiye. Mimi ni wa kwanza, na mimi ni wa mwisho pia.

13  Naam, mkono wangu umeuweka msingi wa dunia, na mkono wangu wa kuume umezitanda mbingu; niziitapo husimama pamoja.

14  Kusanyikeni, ninyi nyote, mkasikie; ni nani miongoni mwao aliyehubiri haya? Bwana amempenda; atatimiza mapenzi yake juu ya Babeli, na mkono wake utakuwa juu ya Wakaldayo.

15  Mimi, naam, mimi, nimenena; naam, nimemwita; nimemleta, naye ataifanikisha njia yake.

16  Nikaribieni, sikieni haya; tokea mwanzo sikunena kwa siri; tangu yalipokuwapo, mimi nipo; na sasa Bwana MUNGU amenituma, na roho yake.

17  Bwana, mkombozi wako, mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Mimi ni Bwana, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata.

18  Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya bahari;

19  Tena wazao wako wangalikuwa kama mchanga, na hao waliotoka katika tumbo lako kama chembe zake; jina lake lisingalikatika, wala kufutwa mbele zangu.

20  Haya, tokeni katika Babeli, Kimbieni kutoka kwa Wakaldayo; Hubirini kwa sauti ya kuimba, tangazeni haya, Yatamkeni mpaka mwisho wa dunia, semeni, Bwana amemkomboa mtumishi wake, Yakobo.

21  Wala hawakuona kiu alipowaongoza jangwani; Alitoa maji katika mwamba kwa ajili yao; Pia akaupasua mwamba, maji yakatoka kwa nguvu.

22  Hapana amani kwa wabaya, asema Bwana.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23