«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Isaya 35

1  Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi.

2  Litachanua maua mengi, na kufurahi, naam, kwa shangwe na kuimba; litapewa uzuri wa Lebanoni, utukufu wa Karmeli na Sharoni; watauona utukufu wa Bwana, ukuu wa Mungu wetu.

3  Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea.

4  Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi.

5  Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa.

6  Ndipo mtu aliye kilema ataruka-ruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba; maana katika nyika maji yatabubujika; na vijito jangwani.

7  Na mchanga ung'aao mfano wa maji utakuwa ziwa la maji, na nchi yenye kiu itakuwa chemchemi za maji; katika makao ya mbweha, walipokuwa wamelala, patakuwa na majani, pamoja na mianzi na manyasi.

8  Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo.

9  Hapo hapatakuwa na simba, wala mnyama mkali hatapanda juu yake; hawataonekana hapo; bali waliokombolewa watakwenda katika njia hiyo.

10  Na hao waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23