«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Hosea 6

1  Njoni, tumrudie Bwana; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga jeraha zetu.

2  Baada ya siku mbili atatufufua; siku ya tatu atatuinua, nasi tutaishi mbele zake.

3  Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua Bwana; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi.

4  Ee Efraimu, nikutendee nini? Ee Yuda, nikutendee nini? Kwa maana fadhili zenu ni kama wingu la asubuhi na kama umande utowekao mapema.

5  Kwa sababu hiyo nimewakata-kata kwa vinywa vya manabii; nimewaua kwa maneno ya kinywa changu; na hukumu yangu itatokea kama mwanga.

6  Maana nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa.

7  Lakini wao wamelivunja hilo agano kama Adamu; huko wamenitenda mambo ya hiana.

8  Gileadi ni mji wa hao watendao maovu, umetiwa rangi ya damu.

9  Na kama vile makundi ya wanyang'anyi wamwoteavyo mtu, ndivyo kundi la makuhani wauavyo katika njia ielekeayo Shekemu; naam, wametenda mambo maovu sana.

10  Katika nyumba ya Israeli nimeona jambo bovu kabisa; huko uzinzi umeonekana katika Efraimu; Israeli ametiwa unajisi.

11  Tena, Ee Yuda, wewe umeandikiwa mavuno, hapo nitakapowarudisha wafungwa wa watu wangu.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23