Hosea 3
1 Bwana akaniambia, Enenda tena, mpende mwanamke apendwaye na rafiki yake, naye ni mzinzi; kama vile Bwana awapendavyo wana wa Israeli, ingawa wanaigeukia miungu mingine, na kupenda mikate ya zabibu kavu.
2 Basi nikajinunulia mwanamke huyo kwa vipande kumi na vitano vya fedha, na homeri moja ya shayiri, na nusu ya homeri ya shayiri;
3 nami nilimwambia, Utatawa kwa ajili yangu siku nyingi; hutafanya mambo ya ukahaba, wala hutakuwa mke wa mtu awaye yote; nami nitakuwa hali iyo hiyo kwa ajili yako.
4 Kwa maana wana wa Israeli watakaa siku nyingi bila mfalme, wala mtu mkuu, wala sadaka, wala nguzo, wala naivera, wala kinyago;
5 baada ya hayo wana wa Israeli watarejea, na kumtafuta Bwana, Mungu wao, na Daudi, mfalme wao; nao watamwendea Bwana na wema wake kwa kicho siku za mwisho.