Hosea 12
1 Efraimu hujilisha upepo, na kuandamana na upepo wa mashariki; haachi kuongeza uongo na uharibifu; nao wafanya agano na Ashuru, na mafuta huchukuliwa kwenda Misri.
2 Bwana naye ana mateto na Yuda, naye atamwadhibu Yakobo kwa kadiri ya njia zake; kwa kadiri ya matendo yake atamlipa.
3 Tumboni alimshika ndugu yake kisigino; Na alipokuwa mtu mzima alikuwa na uwezo kwa Mungu;
4 Naam, alikuwa na uwezo juu ya malaika Akashinda; alilia, na kumsihi; Alimwona huko Betheli, naye akasema nasi huko;
5 Naam, Bwana, Mungu wa majeshi; Bwana ndilo kumbukumbu lake.
6 Basi, mrudie Mungu wako; shika fadhili na hukumu; ukamngojee Mungu wako daima.
7 Ni mchuuzi, mizani ya udanganyifu i mkononi mwake; anapenda kudhulumu.
8 Naye Efraimu alisema, Kweli nimekuwa tajiri, nimejipatia mali nyingi; katika kazi zangu zote hawataona kwangu uovu wo wote uliokuwa dhambi.
9 Lakini mimi ni Bwana, Mungu wako tangu ulipotoka katika nchi ya Misri; nitakukalisha tena katika hema, kama siku za karamu ya idi.
10 Tena nimenena na hao manabii, nami nimeongeza maono, na kwa utumishi wa manabii nimetumia mifano.
11 Je! Gileadi ni uovu? Wamekuwa ubatili tu; huko Gilgali hutoa dhabihu za ng'ombe; naam, madhabahu zao zimekuwa kama chungu katika matuta ya mashamba.
12 Na Yakobo alikimbia mpaka Padan-Aramu, Na Israeli alitumika apate mke; Ili apate mke alichunga kondoo.
13 Na kwa nabii Bwana alimtoa Israeli katika Misri, Na kwa mkono wa nabii alihifadhiwa.
14 Efraimu amenitia hasira kali sana; kwa sababu hiyo damu yake itaachwa juu yake, na Bwana wake atamrudishia lawama yake.