«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Hosea 11

1  Israeli alipokuwa mtoto, nalikuwa nikimpenda, nikamwita mwanangu atoke Misri.

2  Kadiri walivyowaita ndivyo walivyoondoka na kuwaacha; waliwatolea dhabihu Mabaali, na kuzifukizia uvumba sanamu za kuchonga.

3  Lakini nalimfundisha Efraimu kwenda kwa miguu; naliwachukua mikononi mwangu; hawakujua ya kuwa naliwaponya.

4  Naliwavuta kwa kamba za kibinadamu, kwa mafungo ya upendo; nami nalikuwa kwao kama hao waondoao kongwa tayani mwao, nikaandika chakula mbele yao.

5  Hatarudi tena nchi ya Misri; bali huyo Mwashuri atakuwa mfalme wake; kwa sababu walikataa kurejea.

6  Na upanga utaiangukia miji yake, utayaharibu makomeo yake na kuyala, kwa sababu ya mashauri yao wenyewe.

7  Na watu wangu wamejipinda kuniacha; ingawa wawaita kwenda kwake Aliye juu, hapana hata mmoja atakayemtukuza.

8  Niwezeje kukuacha, Efraimu? Niwezeje kukuponya, Israeli? Niwezeje kukufanya kama Adma? Niwezeje kukuweka kama Seboimu ? Moyo wangu umegeuka ndani yangu, huruma zangu zimewaka pamoja.

9  Sitatumia ukali wa hasira yangu, sitarudi kumwangamiza Efraimu; kwa maana mimi ni Mungu, si mwanadamu mimi; mimi ndiye aliye Mtakatifu katikati yenu; wala sitaingia ndani ya mji.

10  Watakwenda kumfuata Bwana, atakayenguruma kama simba; kwa maana atanguruma, nao watoto watakuja kutoka magharibi wakitetemeka.

11  Watakuja wakitetemeka kama shomoro, toka Misri, na kama hua, toka nchi ya Ashuru; nami nitawakalisha katika nyumba zao, asema Bwana.

12  Efraimu amenizinga kwa maneno ya uongo, na nyumba ya Israeli kwa udanganyifu; na Yuda hata sasa anasita-sita kwa Mungu, na kwake aliye Mtakatifu, naye ni mwaminifu.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23