«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Waebrania 3

1  Kwa hiyo, ndugu watakatifu, wenye kuushiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini sana Mtume na Kuhani Mkuu wa maungamo yetu, Yesu,

2  aliyekuwa mwaminifu kwake yeye aliyemweka, kama Musa naye alivyokuwa, katika nyumba yote ya Mungu.

3  Kwa maana huyo amehesabiwa kuwa amestahili utukufu zaidi kuliko Musa, kama vile yeye aitengenezaye nyumba alivyo na heshima zaidi ya hiyo nyumba.

4  Maana kila nyumba imetengenezwa na mtu; ila yeye aliyevitengeneza vitu vyote ni Mungu.

5  Na Musa kweli alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu kama mtumishi, awe ushuhuda wa mambo yatakayonenwa baadaye;

6  bali Kristo, kama mwana, juu ya nyumba ya Mungu; ambaye nyumba yake ni sisi, kama tukishikamana sana na ujasiri wetu na fahari ya taraja letu mpaka mwisho.

7  Kwa hiyo, kama anenavyo Roho Mtakatifu, Leo, kama mtaisikia sauti yake,

8  Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha, Siku ya kujaribiwa katika jangwa,

9  Hapo baba zenu waliponijaribu, wakanipima, Wakaona matendo yangu miaka arobaini.

10  Kwa hiyo nalichukizwa na kizazi hiki, Nikasema, Sikuzote ni watu waliopotoka mioyo hawa; Hawakuzijua njia zangu;

11  Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu.

12  Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai.

13  Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.

14  Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho;

15  hapo inenwapo, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha.

16  Maana ni akina nani waliokasirisha, waliposikia? Si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Musa?

17  Tena ni akina nani aliochukizwa nao miaka arobaini? Si wale waliokosa, ambao mizoga yao ilianguka katika jangwa?

18  Tena ni akina nani aliowaapia ya kwamba hawataingia katika raha yake, ila wale walioasi?

19  Basi twaona ya kuwa hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23