«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Habakuki 3

1  Sala ya nabii Habakuki.

2  Ee Bwana, nimesikia habari zako, nami naogopa; Ee Bwana, fufua kazi yako katikati ya miaka; Katikati ya miaka tangaza habari yake; Katika ghadhabu kumbuka rehema.

3  Mungu alikuja kutoka Temani, Yeye aliye mtakatifu kutoka mlima Parani. Utukufu wake ukazifunika mbingu, Nayo dunia ikajaa sifa yake.

4  Mwangaza wake ulikuwa kama nuru; Alikuwa na mishale ya nuru ubavuni pake; Ndipo ulipofichwa uweza wake.

5  Mbele zake ilikwenda tauni, Na makaa ya moto yakatoka miguuni pake.

6  Akasimama, akaitetemesha dunia; Akatazama, akawasitusha mataifa; Na milima ya zamani ikatawanyika; Vilima vya kale vikainama; Miendo yake ilikuwa kama siku za kale.

7  Naliziona hema za Kushani katika taabu; Mapazia ya nchi ya Midiani yakatetemeka.

8  Je! Bwana aliikasirikia mito? Je! Hasira yako ilikuwa juu ya mito, Au ghadhabu yako juu ya bahari, Hata ukapanda farasi zako, Katika magari yako ya wokovu?

9  Uta wako ukafanywa wazi kabisa; Viapo walivyopewa kabila vilikuwa neno thabiti; Ukaipasua nchi kwa mito.

10  Milima ilikuona, ikaogopa; Gharika ya maji ikapita; Vilindi vikatoa sauti yake, Vikainua juu mikono yake.

11  Jua na mwezi vikasimama makaoni mwao; Mbele ya nuru ya mishale yako ilipotapakaa, Mbele ya mwangaza wa mkuki wako umeremetao.

12  Ulikwenda katikati ya nchi kwa ghadhabu; Ukawapura mataifa kwa hasira.

13  Ukatokea kwa ajili ya wokovu wa watu wako, Kwa ajili ya wokovu wa masihi

14  Ukakichoma kichwa cha mashujaa wake kwa fimbo zao wenyewe; Wakaja kama kisulisuli ili kunitawanya; Kama wakifurahi kuwameza maskini kwa siri.

15  Ukaikanyaga bahari kwa farasi zako, Chungu ya maji yenye nguvu.

16  Nikasikia, na tumbo langu likatetemeka, Midomo yangu ikatikisika kwa sauti ile; Ubovu ukaingia mifupani mwangu, Nikatetemeka katika mahali pangu; Ili nipate kuingoja ile siku ya dhiki, Kundi lao washambuliao wakweapo juu ya watu.

17  Maana mtini hautachanua maua, Wala mizabibuni hamtakuwa na matunda; Taabu ya mzeituni itakuwa bure, Na mashamba hayatatoa chakula; Zizini hamtakuwa na kundi, Wala vibandani hamtakuwa na kundi la ng'ombe;

18  Walakini nitamfurahia Bwana Nitamshangilia Mungu wa wokovu wangu.

19  YEHOVA, aliye Bwana, ni nguvu zangu, Yeye huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu, Naye ataniendesha katika mahali pangu palipoinuka.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23