Wagalatia 3
1 Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa?
2 Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?
3 Je! Mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho, mnataka kukamilishwa sasa katika mwili?
4 Mmepatikana na mateso makubwa namna hii bure? Ikiwa ni bure kweli.
5 Basi, yeye awapaye Roho na kufanya miujiza kati yenu, je! Afanya hayo kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?
6 Kama vile Ibrahimu alivyomwamini Mungu akahesabiwa haki.
7 Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu.
8 Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa.
9 Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwenye imani.
10 Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye.
11 Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani.
12 Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo.
13 Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti;
14 ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.
15 Ndugu zangu, nanena kwa jinsi ya kibinadamu. Lijapokuwa ni agano la mwanadamu, hata hivyo likiisha kuthibitika, hakuna mtu alibatilishaye, wala kuliongeza neno.
16 Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo.
17 Nisemalo ni hili; agano lililothibitishwa kwanza na Mungu, torati iliyotokea miaka mia nne na thelathini baadaye hailitangui, hata kuibatilisha ile ahadi.
18 Kwa maana urithi ukiwa kwa sheria, hauwi tena kwa ahadi; lakini Mungu alimkirimia Ibrahimu kwa njia ya ahadi.
19 Torati ni nini basi? Iliingizwa kwa sababu ya makosa, hata aje huyo mzao aliyepewa ile ahadi; iliamriwa kwa utumishi wa malaika kwa mkono wa mjumbe.
20 Basi aliye mjumbe si mjumbe wa mmoja; bali Mungu ni mmoja.
21 Basi je! Torati haipatani na ahadi za Mungu? Hasha! Kwa kuwa, kama ingalitolewa sheria iwezayo kuhuisha, yakini haki ingalipatikana kwa sheria.
22 Lakini andiko limeyafunga yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile ahadi kwa imani ya Yesu Kristo.
23 Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa.
24 Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani.
25 Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi.
26 Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu.
27 Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo.
28 Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu.
29 Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.