Ezra 4
1 Basi adui za Yuda na Benyamini, waliposikia ya kuwa wana wa uhamisho wanamjengea Bwana, Mungu wa Israeli, hekalu,
2 wakamkaribia Zerubabeli, na wakuu wa mbari za mababa, wakawaambia, Na tujenge sisi nasi pamoja nanyi; kwa maana tunamtafuta Mungu wenu kama ninyi, nasi twamtolea dhabihu tangu zamani za Esar-hadoni, mfalme wa Ashuru, aliyetupandisha mpaka hapa.
3 Lakini Zerubabeli, na Yoshua, na wakuu wengine wa mbari za mababa katika Israeli, wakawaambia, Ninyi haiwahusu kushirikiana nasi katika kumjengea Mungu wetu nyumba; bali sisi wenyewe peke yetu tutamjengea Bwana, Mungu wa Israeli, nyumba, kama mfalme Koreshi, mfalme wa Uajemi, alivyotuamuru.
4 Ndipo watu wa nchi wakaidhoofisha mikono ya watu wa Yuda, wakawasumbua, walipokuwa wakijenga.
5 Wakawaajiri washauri juu yao, ili kuwapinga kusudi lao, siku zote za Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata wakati wa kutawala kwake Dario, mfalme wa Uajemi.
6 Tena, wakati wa kutawala kwake Ahasuero, mwanzo wa kutawala kwake, watu wakaandika mashitaka juu ya wenyeji wa Yuda na Yerusalemu.
7 Na tena, katika siku za Artashasta, Mithredathi, na Tabeeli na mabaki ya wenziwe, wakimwandikia Artashasta, mfalme wa Uajemi, salamu za heri; na mwandiko wa waraka huo, ukaandikwa kwa herufi za Kiaramu, na kunenwa kwa lugha ya Kiaramu.
8 Nao Rehumu, Bwana shauri, na Shimshai, mwandishi, wakaandika waraka juu ya Yerusalemu kwa Artashasta, mfalme, kama hivi;
9 Rehumu, Bwana shauri, na Shimshai, mwandishi, na mabaki ya wenzao, makadhi wa Kiajemi na madiwani wa Kiajemi; na Waarkewi, Wababeli, Washushani, yaani, Waelami;
10 na mabaki ya mataifa, ambao Asur-bani-pali mkuu, mwenye heshima, aliwavusha, na kuwakalisha katika mji wa Samaria, na mahali penginepo, ng'ambo ya Mto; wakadhalika.
11 Hii ndiyo nakili ya waraka waliyompelekea mfalme Artashasta;
12 Ijulikane kwa mfalme ya kuwa Wayahudi, waliokwea kutoka kwako, wamefika kwetu Yerusalemu; nao wanaujenga ule mji mwasi, mbaya; wamemaliza kuta zake, na kuitengeneza misingi yake.
13 Basi, ijulikane kwa mfalme, ya kuwa mji huu ukijengwa, na kuta zake zikimalizika, hawatatoa kodi, wala ada, wala ushuru, na mwisho wake wafalme watapata hasara.
14 Na sisi, kwa kuwa tunakula chumvi ya nyumba ya mfalme, wala si wajibu wetu kumwona mfalme akivunjiwa heshima, basi tumetuma watu na kumwarifu mfalme.
15 Ili habari zitafutwe katika kitabu cha tarehe za baba zako; ndivyo utakavyopata kujua kwa kitabu cha tarehe ya kuwa mji huo ni mji mwasi, wenye kuwadhuru wafalme, na maliwali, na ya kuwa wenyeji wake wamefanya fitina katika mji huo zamani; ndiyo sababu mji huo ukaangamizwa.
16 Twamwarifu mfalme ya kuwa mji huo ukijengwa, na kuta zake zikimalizika, hutakuwa na sehemu ya nchi ng'ambo ya Mto.
17 Ndipo mfalme akapeleka majibu;
18 Ule waraka mlionipelekea umesomwa mbele yangu, nami nikaelewa na maana yake.
19 Nikatoa amri, na watu wametafuta habari; ikaonekana ya kuwa mji huu zamani umefanya fitina juu ya wafalme, na ya kuwa uasi na fitina zimefanyika ndani yake.
20 Tena walikuwako wafalme wakuu juu ya Yerusalemu, waliotawala nchi yote iliyo ng'ambo ya Mto; wakapewa kodi, na ada, na ushuru.
21 Sasa toeni amri kuwakomesha watu hawa kazi yao, mji huu usijengwe, hata mimi nitakapotoa amri.
22 Tena jihadharini, msilegee katika jambo hili; kwa nini madhara yazidi, na wafalme wapate hasara?
23 Hata nakala ya waraka huo wa mfalme Artashasta uliposomwa mbele ya Rehumu, Bwana shauri, na Shimshai, mwandishi, na wenzao, wakaenda Yerusalemu upesi, kwa Wayahudi, wakawakomesha kwa nguvu na kwa kuwashurutisha.
24 Hivyo kazi ya nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu ikakoma; nayo ikakoma hata mwaka wa pili wa kutawala kwake Dario, mfalme wa Uajemi.