«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Ezekieli 9

1  Kisha akalia kwa sauti kuu masikioni mwangu, akisema, Waamuru wale wanaousimamia mji wakaribie, kila mmoja na awe na kitu chake cha kuangamiza mkononi mwake.

2  Na tazama, watu sita wakaja, wakitokea kwa njia ya lango la juu, lielekealo upande wa kaskazini, kila mmoja ana kitu chake cha kufisha mkononi mwake; na mtu mmoja kati yao amevaa bafta, naye ana kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. Wakaingia, wakasimama karibu na madhabahu ya shaba.

3  Na huo utukufu wa Bwana wa Israeli ulikuwa umepanda juu kutoka kwa kerubi, ambaye ulikuwa juu yake, mpaka kizingiti cha nyumba; akamwita mtu yule aliyekuwa amevaa bafta, mwenye kidau cha wino cha mwandishi kiunoni.

4  Bwana akamwambia, Pita kati ya mji, kati ya Yerusalemu, ukatie alama katika vipaji vya nyuso vya watu wanaougua na kulia kwa sababu ya machukizo yote yanayofanyika kati yake.

5  Na hao wengine aliwaambia, nami nalisikia, Piteni kati ya mji nyuma yake, mkapige; jicho lenu lisiachilie, wala msione huruma;

6  Waueni kabisa, mzee, na kijana, na msichana, na watoto wachanga, na wanawake; lakini msimkaribie mtu ye yote mwenye hiyo alama; tena anzeni katika patakatifu pangu. Basi, wakaanza kwa wazee waliokuwa mbele ya nyumba.

7  Akawaambia, itieni nyumba unajisi, mkazijaze nyua mizoga ya hao waliouawa; haya, enendeni. Wakaenenda, wakapiga-piga katika mji.

8  Tena ikawa, walipokuwa wakipiga, nami nikiachwa, nalianguka kifudifudi, nikalia, nikasema, Ee Bwana MUNGU! Utaangamiza mabaki yote ya Israeli, wakati wa kumwaga ghadhabu yako juu ya Yerusalemu?

9  Ndipo akaniambia, Uovu wa nyumba ya Israeli na Yuda ni mwingi sana, nayo nchi imejaa damu, nao mji umejaa kupotosha hukumu; maana husema, Bwana ameiacha nchi hii, naye Bwana haoni.

10  Nami, jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; lakini nitaleta njia yao juu ya vichwa vyao.

11  Na tazama, mtu yule aliyevaa bafta, mwenye kidau cha wino kiunoni, akaleta habari, akisema, Nimefanya kama ulivyoniamuru.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23