«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Ezekieli 25

1  Neno la Bwana likanijia, kusema,

2  Mwanadamu, uwaelekezee wana wa Amoni uso wako, ukatabiri juu yao.

3  Uwaambie hao wana wa Amoni, Lisikieni neno la Bwana MUNGU; Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu umesema, Aha! Juu ya patakatifu pangu, palipotiwa unajisi; na juu ya nchi ya Israeli, ilipoharibiwa; na juu ya nyumba ya Israeli, walipokwenda kifungoni;

4  basi, kwa sababu hiyo, nitakutia katika mikono ya wana wa mashariki uwe milki yao, nao wataweka marago yao ndani yako, kufanya maskani zao ndani yako; watakula matunda yako, na kunywa maziwa yako.

5  Nami nitafanya Raba kuwa banda la ngamia, na wana wa Amoni kuwa mahali pa kulaza makundi; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

6  Maana Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu umepiga makofi, na kupiga mshindo kwa miguu yako, na kufurahi juu ya nchi ya Israeli, jeuri yote ya roho yako;

7  basi, tazama, nimenyosha mkono wangu juu yako, nami nitakutoa uwe mateka ya mataifa; nami nitakukatilia mbali na kabila za watu, nami nitakuangamiza, usiwe katika nchi hizo; nitakukomesha; nawe utajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

8  Bwana MUNGU asema hivi; Kwa sababu Moabu na Seiri husema, Tazama, nyumba ya Israeli ni sawasawa na mataifa yote;

9  basi, tazama, nitawafunulia wana wa mashariki ubavu wa Moabu toka miji yake, toka miji yake iliyo mipakani mwake, utukufu wa nchi hiyo, Beth-yeshimothi, na Baal-meoni, na Kiriathaimu,

10  pamoja na wana wa Amoni, nami nitawatoa kuwa milki, ili wana wa Amoni wasikumbukwe kati ya mataifa,

11  nami nitatoa hukumu juu ya Moabu; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

12  Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa Edomu wametenda kinyume cha nyumba ya Yuda, kwa kujilipiza kisasi, nao wamekosa sana, na kujilipiza kisasi juu yao;

13  kwa sababu hiyo, Bwana MUNGU asema hivi; Nitanyosha mkono wangu juu ya Edomu, nitakatilia mbali nayo wanadamu na wanyama; nami nitaifanya kuwa ukiwa toka Temani; na mpaka Dedani wataanguka kwa upanga.

14  Nami nitaweka kisasi changu juu ya Edomu, kwa mkono wa watu wangu Israeli; nao watatenda mambo katika Edomu, kwa kadiri ya hasira yangu, na ghadhabu yangu, nao watakijua kisasi changu, asema Bwana MUNGU.

15  Bwana MUNGU asema hivi; Kwa kuwa Wafilisti wametenda mambo kwa kujilipiza kisasi, nao wamejilipiza kisasi kwa jeuri ya roho, ili kupaangamiza kwa uadui wa daima;

16  kwa sababu hiyo, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, nitanyosha mkono wangu juu ya Wafilisti, nami nitawakatilia mbali Wakerethi, na kuwaharibu wabakio pande za pwani.

17  Nami nitajilipiza kisasi kikuu, nikiwakemea kwa ukali; nao watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapojilipiza kisasi juu yao.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23