«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Ezekieli 2

1  Akaniambia, Mwanadamu, simama kwa miguu yako, nami nitasema nawe.

2  Naye aliposema nami, roho ikaniingia, ikanisimamisha; nikamsikia yeye aliyesema nami.

3  Akaniambia, Mwanadamu, nakutuma kwa wana wa Israeli, kwa mataifa wanaoasi, walioniasi mimi; wao na baba zao wamekosa juu yangu, naam, hata hivi leo.

4  Na wana hao wana nyuso zisizo na haya, na mioyo yao ni migumu. Mimi nakutuma kwa hao; nawe utawaambia, Bwana MUNGU asema hivi.

5  Nao, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia, (maana ndio nyumba ya kuasi hao), hata hivyo watajua ya kuwa nabii amekuwako miongoni mwao.

6  Na wewe, mwanadamu, usiwaogope hao, wala usiyaogope maneno yao, ijapokuwa miiba na michongoma i pamoja nawe, nawe unakaa katikati ya nge; usiyaogope maneno yao, wala usifadhaike kwa sababu ya nyuso zao, wajapokuwa ni nyumba yenye kuasi.

7  Nawe utawaambia maneno yangu, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia; maana hao wanaasi sana.

8  Bali wewe, mwanadamu, sikia neno hili ninalokuambia; usiwe wewe mwenye kuasi kama nyumba ile yenye kuasi; funua kinywa chako, ule nikupacho.

9  Nami nilipotazama, mkono ulinyoshwa kunielekea; na tazama, gombo la chuo lilikuwa ndani yake.

10  Akalikunjua mbele yangu; nalo lilikuwa limeandikwa ndani na nje; ndani yake yalikuwa yameandikwa maombolezo, na vilio, na ole!

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23