«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Ezekieli 14

1  Ndipo baadhi ya wazee wa Israeli wakanijia, wakaketi mbele yangu.

2  Ndipo neno la Bwana likanijia, kusema,

3  Mwanadamu, watu hawa wametwaa vinyago vyao na kuvitia mioyoni mwao, nao wameweka kwazo la uovu wao mbele ya nyuso zao. Je! Ni laiki yangu niulizwe na wao katika neno lo lote?

4  Basi sema nao, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Kila mtu wa nyumba ya Israeli atwaaye vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, na kumwendea nabii; mimi, Bwana, nitamjibu neno lake sawasawa na wingi wa sanamu zake;

5  ili niwakamate nyumba ya Israeli kwa mioyo yao wenyewe, kwa sababu wamefarakana nami kwa vinyago vyao.

6  Kwa sababu hiyo uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana MUNGU asema hivi; Rudini ninyi, mkageuke na kuviacha vinyago vyenu; mkageuze nyuso zenu zisielekee machukizo yenu yote.

7  Kwa maana kila mtu wa nyumba ya Israeli, au wa wageni wakaao katika Israeli, ajitengaye nami, na kuvitwaa vinyago vyake na kuvitia moyoni mwake, na kuliweka kwazo la uovu wake mbele ya uso wake, kisha kumwendea nabii, na kuniuliza neno kwa ajili ya nafsi yake; mimi, Bwana, nitamjibu, mimi mwenyewe;

8  nami nitaukaza uso wangu juu ya mtu yule, na kumfanya kuwa ajabu, awe ishara na mithali, nami nitamkatilia mbali, asiwe kati ya watu wangu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.

9  Na nabii akidanganyika, na kusema neno, mimi, Bwana, nimemdanganya nabii yule, nami nitaunyosha mkono wangu juu yake, na kumwangamiza, asiwe kati ya watu wangu Israeli.

10  Nao watauchukua uovu wao; uovu wa nabii utakuwa sawasawa na uovu wake yule amwendeaye aulize neno;

11  ili nyumba ya Israeli wasipotee mbali nami, wala wasijitie unajisi tena kwa makosa yao yote; bali wawe watu wangu, nami niwe Mungu wao, asema Bwana MUNGU.

12  Neno la Bwana likanijia, kusema,

13  Mwanadamu, nchi itakapofanya dhambi na kuniasi, kwa kukosa, nikaunyosha mkono wangu juu yake, na kulivunja tegemeo la chakula chake, na kuipelekea njaa, na kukatilia mbali mwanadamu na mnyama;

14  wajapokuwa watu hawa watatu, Nuhu, na Danieli, na Ayubu, kuwamo ndani yake, wangejiokoa nafsi zao wenyewe tu kwa haki yao, asema Bwana MUNGU.

15  Nikipitisha wanyama wabaya ndani ya nchi ile, wakaiharibu hata ikawa ukiwa, mtu awaye yote asiweze kupita ndani yake, kwa sababu ya wanyama hao;

16  wajapokuwamo watu hawa watatu ndani yake, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala binti; wao wenyewe tu wataokoka, bali nchi ile itakuwa ukiwa.

17  Au nikileta upanga juu ya nchi ile, na kusema, Upanga, pita kati ya nchi hii, hata nikawakatilia mbali na nchi hiyo wanadamu na wanyama;

18  wajapokuwamo watu hawa watatu ndani yake, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala binti; bali wao wenyewe tu wataokoka.

19  Au nikipeleka tauni katika nchi ile, na kumwaga ghadhabu yangu juu yake, kwa damu; ili kuwakatilia mbali nayo wanadamu na wanyama;

20  wajapokuwamo ndani yake Nuhu, na Danieli, na Ayubu, kama mimi niishivyo, asema Bwana MUNGU, hawataokoa wana wala binti; watajiokoa nafsi zao tu kwa haki yao.

21  Maana Bwana MUNGU asema hivi; Je! U zaidi sana nitakapoleta hukumu zangu nne zilizo kali juu ya Yerusalemu, yaani, upanga, na njaa, na wanyama wabaya, na tauni, niwakatilie mbali nayo wanadamu na wanyama?

22  Lakini, tazama, watasalia mabaki watakaochukuliwa nje, wana na binti; tazama, watawatokea ninyi, nanyi mtaiona njia yao na matendo yao; nanyi mtafarijika katika habari ya mabaya niliyoleta juu ya Yerusalemu, naam, katika habari ya mambo yote niliyoleta juu yake.

23  Nao watawafariji ninyi, mtakapoona njia yao na matendo yao; nanyi mtajua ya kuwa sikufanya bila sababu mambo yote niliyoutenda, asema Bwana MUNGU.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23