«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Kutoka 18

1  Basi Yethro, kuhani wa Midiani, mkwewe Musa, alisikia habari ya mambo hayo yote Mungu aliyokuwa amemtendea Musa, na Waisraeli watu wake, jinsi Bwana alivyowaleta Israeli watoke Misri.

2  Ndipo Yethro mkwewe Musa akamtwaa Sipora, mke wa Musa, baada ya yeye kumrudisha,

3  pamoja na wanawe wawili; katika hao, jina la mmoja ni Gershomu, maana alisema, Mimi nimekuwa mgeni katika nchi ya ugenini;

4  na jina la wa pili ni Eliezeri, kwa kuwa alisema, Yeye Mungu wa baba yangu alikuwa msaada wangu, akaniokoa na upanga wa Farao.

5  Basi Yethro, mkwewe Musa, pamoja na mke wa Musa na wanawe wawili wakamwendea Musa huko nyikani, hapo alipokuwa amepanga, kwenye mlima wa Mungu;

6  naye akamwambia Musa, Mimi Yethro mkweo nimekuja kwako, na mkeo, na wanawe wawili pamoja naye.

7  Basi Musa akatoka nje ili amlaki mkwewe, akasujudia na kumbusu; nao wakaulizana habari; kisha wakaingia hemani.

8  Musa akamwambia mkwewe mambo hayo yote Bwana aliyomtenda Farao na Wamisri kwa ajili ya Israeli, na mambo mazito yote yaliyowapata njiani, na jinsi Bwana alivyowaokoa.

9  Yethro alifurahi kwa ajili ya wema wote Bwana aliowatendea Israeli, kwa alivyo waokoa mikononi mwa Wamisri.

10  Kisha Yethro akasema, Na ahimidiwe Bwana aliyewaokoa na mikono ya Wamisri, na mkono wa Farao; aliyewaokoa watu hao watoke mikononi mwa Wamisri.

11  Sasa najua ya kuwa Bwana ni mkuu kuliko miungu yote; naam, katika jambo hilo walilowatenda kwa unyeti.

12  Yethro mkwewe Musa akamletea Mungu sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; na Haruni akaja, na wazee wote wa Israeli, wale chakula pamoja na mkwewe Musa mbele za Mungu.

13  Asubuhi yake Musa akaketi ili awapishie hukumu watu; na hao watu wakasimama kumzunguka Musa tangu asubuhi hata jioni.

14  Mkwewe Musa alipoyaona yote aliyowafanyia watu, akasema, Ni jambo gani hili uwatendealo hao watu? Kwani wewe kuketi hapo peke yako, na watu wote kusimama kwako tangu asubuhi hata jioni?

15  Musa akamwambia mkwewe, Ni kwa sababu watu hunijilia mimi wapate kumwuliza Mungu;

16  wakiwa na neno, hunijilia; nami naamua kati ya mtu na mwenziwe, nami nawajuvisha amri za Mungu, na sheria zake.

17  Mkwewe Musa akamwambia, Jambo hili ufanyalo si jema.

18  Huna budi utadhoofika wewe, na hawa watu walio pamoja nawe pia; maana jambo hili ni zito mno kwako; huwezi wewe kulitenda peke yako.

19  Sikiza sasa neno langu, nitakupa shauri, na Mungu na awe pamoja nawe; uwe wewe kwa ajili ya watu mbele ya Mungu, nawe umletee Mungu maneno yao;

20  nawe utawafundisha zile amri na sheria, nawe utawaonyesha njia ambayo inawapasa kuiendea, na kazi ambayo inawapasa kuifanya.

21  Zaidi ya hayo utajipatia katika watu hawa watu walio na uwezo, wenye kumcha Mungu, watu wa kweli, wenye kuchukia mapato ya udhalimu; ukawaweka juu yao, wawe wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi;

22  nao wawaamue watu hawa sikuzote; kisha, kila neno lililo kubwa watakuletea wewe, lakini kila neno dogo wataliamua wenyewe; basi kwako wewe mwenyewe utapata nafasi zaidi, nao watauchukua huo mzigo pamoja nawe.

23  Kwamba utafanya jambo hili, na Mungu akikuagiza hivyo, basi utaweza kusimama wewe, na watu hawa wote nao watakwenda mahali pao kwa amani.

24  Basi Musa akasikiza neno la mkwewe, akayafanya yote aliyokuwa amemwambia.

25  Musa akawachagua watu wenye uwezo katika Israeli yote, akawaweka wawe vichwa juu ya watu, wakuu wa maelfu, na wakuu wa mia, na wakuu wa hamsini, na wakuu wa kumi.

26  Nao wakawaamua watu sikuzote; mashauri magumu wakamletea Musa, lakini kila neno dogo wakaliamua wenyewe.

27  Kisha Musa akaagana na mkwewe; naye akaenda zake, mpaka nchi yake mwenyewe.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23