«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Kumbukumbu la Torati 34

1  Musa akapanda kutoka uwanda wa Moabu mpaka mlima Nebo, hata kilele cha Pisga kukabili Yeriko. Bwana akamwonyesha nchi yote ya Gileadi hata Dani;

2  na Naftali yote, na nchi ya Efraimu na Manase, na nchi yote ya Yuda, mpaka bahari ya magharibi;

3  na Negebu, na uwanja wa bonde la Yeriko, mji wa mitende, hata mpaka Soari.

4  Bwana akamwambia, Hii ndiyo nchi niliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, nikisema, Nitawapa wazao wako. Basi nimekuonyesha kwa macho yako, lakini hutavuka huko.

5  Basi Musa, mtumishi wa Bwana, akafa huko, katika nchi ya Moabu, kwa neno la Bwana.

6  Akamzika bondeni, katika nchi ya Moabu, kukabili Beth-peori; lakini hapana mtu ajuaye kaburi lake hata leo.

7  Musa alikuwa mtu wa miaka mia na ishirini alipokufa; jicho lake halikupofuka, wala nguvu za mwili wake hazikupunguka.

8  Wana wa Israeli wakamwombolezea Musa katika uwanda wa Moabu siku thelathini; basi siku za maombolezo ya matanga ya Musa zikaisha.

9  Na Yoshua, mwana wa Nuni, alikuwa amejaa roho ya hekima; maana Musa alikuwa amemwekea mikono yake juu yake; wana wa Israeli wakamsikiliza, wakafanya kama Bwana alivyomwamuru Musa.

10  Wala hajainuka tena katika Israeli nabii kama Musa, ambaye Bwana alimjua uso kwa uso;

11  katika ishara zote na maajabu yote, ambayo Bwana alimtuma kuyatenda katika nchi ya Misri, kwa Farao, na kwa watumishi wake wote, na kwa nchi yake yote;

12  na katika ule mkono wa nguvu wote, tena katika ule utisho mkuu wote, alioutenda Musa machoni pa Israeli wote.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23