Danieli 12
1 Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo; na wakati huo watu wako wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile.
2 Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele.
3 Na walio na hekima watang'aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele.
4 Lakini wewe, Ee Danieli, yafunge maneno haya, ukakitie muhuri kitabu, hata wakati wa mwisho; wengi wataenda mbio huko na huko, na maarifa yataongezeka.
5 Ndipo mimi, Danieli, nikatazama, na kumbe, wamesimama wengine wawili, mmoja ukingoni mwa mto upande huu, na mmoja ukingoni mwa mto upande wa pili.
6 Na mmoja akamwuliza yule mtu aliyevikwa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, Je! Itakuwa muda wa miaka mingapi hata mwisho wa mambo haya ya ajabu?
7 Nami nikamsikia yule mtu aliyevikwa nguo za kitani, aliyekuwa juu ya maji ya mto, hapo alipoinua mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto kuelekea mbinguni; akaapa kwa yeye aliye hai milele na milele, ya kwamba itakuwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati; tena watakapokuwa wamekwisha kuvunja nguvu za hao watu watakatifu, ndipo mambo hayo yote yatakapotimizwa.
8 Nami nikasikia, lakini sikuelewa; ndipo nikasema, Ee Bwana wangu, mwisho wa mambo haya utakuwaje?
9 Akasema, Enenda zako, Danieli; maana maneno haya yamefungwa, na kutiwa muhuri, hata wakati wa mwisho.
10 Wengi watajitakasa, na kujifanya weupe, na kusafika; bali wabaya watatenda mabaya; wala hataelewa mtu mbaya awaye yote; bali wao walio na hekima ndio watakaoelewa.
11 Na tangu wakati ule ambapo sadaka ya kuteketezwa ya daima itaondolewa, na hilo chukizo la uharibifu litakaposimamishwa, itapata siku elfu na mia mbili na tisini.
12 Heri angojaye, na kuzifikilia siku hizo elfu na mia tatu na thelathini na tano.
13 Lakini enenda zako hata utakapokuwa mwisho ule; maana wewe utastarehe, nawe utasimama katika kura yako mwisho wa siku hizo.