Amosi 6
1 Ole wao wanaostarehe katika Sayuni, na hao wanaokaa salama katika mlima wa Samaria, watu mashuhuri wa taifa lililo la kwanza, ambao nyumba ya Israeli huwaendea.
2 Piteni hata Kalne, mkaone; tena tokea huko enendeni hata Hamathi iliyo kuu; kisha shukeni hata Gathi ya Wafilisti; je! Ninyi ni bora kuliko falme hizi? Au mpaka wao ni mkubwa kuliko mpaka wenu?
3 Ninyi mnaoiweka mbali siku hiyo mbaya, na kulileta karibu kao la udhalimu;
4 ninyi mnaolala juu ya vitanda vya pembe, na kujinyosha juu ya masemadari yenu; ninyi mnaokula wana-kondoo wa kundi, na ndama waliomo zizini;
5 ninyi mnaoimba nyimbo za upuzi pamoja na sauti ya vinanda, na kujifanyizia vinanda vya namna nyingi, kama vile Daudi;
6 ninyi mnaokunywa divai katika mabakuli, na kujipaka marhamu iliyo nzuri; lakini hawahuzuniki kwa sababu ya mateso ya Yusufu.
7 Basi kwa ajili ya hayo sasa watakwenda utumwani pamoja na wa kwanza watakaokwenda utumwani, na kelele za machezo za hao waliojinyosha zitakoma.
8 Bwana MUNGU ameapa kwa nafsi yake, asema Bwana, Mungu wa majeshi; Naizira fahari ya Yakobo, nachukizwa na majumba yake; kwa sababu hiyo nitautoa huo mji, pamoja na wote waliomo ndani yake.
9 Hata itakuwa, wakisalia wanaume kumi katika nyumba moja, watakufa.
10 Na mjomba wa mtu atakapomwinua, yaani, yeye amchomaye moto, ili atoe mifupa yake nyumbani, naye atakapomwambia yeye aliye katika pande za ndani za nyumba, Je! Yuko mtu ye yote pamoja nawe? Naye atakaposema, La, hapana; ndipo atasema, Nyamaza kimya; maana hatuna ruhusa kulitaja jina la Bwana.
11 Kwa maana, angalia, Bwana atoa amri, na nyumba kubwa itapigwa na kuwa na mahali palipobomolewa, na nyumba ndogo nayo itapigwa iwe na nyufa.
12 Je! Farasi watapiga mbio juu ya mwamba? Je! Mtu atalima na ng'ombe huko? Hata mmegeuza hukumu kuwa uchungu, na matunda ya haki kuwa pakanga;
13 ninyi mnaolifurahia jambo lisilo na maana, msemao, Je! Hatukujipatia pembe kwa nguvu zetu wenyewe?
14 Maana, angalia, nitaondokesha taifa juu yenu, enyi nyumba ya Israeli, asema Bwana, Mungu wa majeshi, nao watawatesa ninyi toka mahali pa kuingilia katika Hamathi hata kijito cha Araba.