«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Amosi 4

1  Lisikieni neno hili, enyi ng'ombe wa Bashani, mnaokaa juu ya mlima wa Samaria, mnaowaonea maskini, na kuwaponda wahitaji; mnaowaambia bwana zao, Haya! Leteni, tunywe.

2  Bwana MUNGU ameapa kwa utakatifu wake, ya kuwa, tazama, siku zitawajilia, watakapowaondoa ninyi kwa kulabu, na mabaki yenu kwa ndoana.

3  Nanyi mtatoka kwenye mahali palipobomolewa, kila mwanamke moja kwa moja mbele yake; nanyi mtajitupa katika Harmoni, asema Bwana.

4  Njoni Betheli, mkakose; njoni Gilgali, mkaongeze makosa; kaleteni dhabihu zenu kila asubuhi, na zaka zenu kila siku ya tatu;

5  mkachome sadaka ya shukrani, ya kitu kilichotiwa chachu; mkatangaze sadaka mtoazo kwa hiari na kuzihubiri habari zake; kwa maana ndivyo viwapendezavyo ninyi, enyi wana wa Israeli, asema Bwana MUNGU.

6  Mimi nami nimewapa usafi wa meno katika miji yenu yote, na kutindikiwa na mkate mahali penu pote; lakini hamkunirudia mimi, asema Bwana.

7  Tena nimeizuia mvua msiipate, ilipobaki miezi mitatu kabla ya mavuno; nami nimenyesha mvua juu ya mji mmoja, nikaizuia mvua isinyeshe juu ya mji mwingine; sehemu moja ilipata mvua, na sehemu isiyopata mvua ilikatika.

8  Basi kutoka miji miwili mitatu walitanga-tanga kuendea mji mwingine wapate kunywa maji, wasipate ya kuwatosha; lakini hamkunirudia mimi, asema Bwana.

9  Nami nimewapiga kwa ukavu na koga; wingi wa bustani zenu na mashamba yenu ya mizabibu, na mitini yenu na mizeituni yenu imeliwa na tunutu; Lakini hamkunirudia mimi, asema Bwana.

10  Nimewapelekea tauni, kama tauni ya Misri; vijana wenu nimewaua kwa upanga, na farasi wenu nimewachukulia mbali; nami nimeupandisha uvundo wa matuo yenu na kuuingiza katika mianzi ya pua zenu; lakini hamkunirudia mimi, asema Bwana.

11  Baadhi yenu nimewaangamiza, kama hapo Mungu alipoiangamiza Sodoma na Gomora, nanyi mkawa kama kinga kilichonyakuliwa motoni; lakini hamkunirudia mimi, asema Bwana.

12  Basi nitakutenda hivi, Ee Israeli, na kwa sababu nitakutenda hivi, ujiweke tayari kuonana na Mungu wako, Ee Israeli.

13  Kwa maana, angalia, yeye aifanyizaye milima, na kuuumba upepo, na kumwambia mwanadamu mawazo yake, afanyaye asubuhi kuwa giza, na kupakanyaga mahali pa dunia palipoinuka; Bwana, Mungu wa majeshi, ndilo jina lake.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23