«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

Amosi 1

1  Maneno ya Amosi, aliyekuwa mmoja wa wachungaji wa Tekoa; maono aliyoyaona katika habari za Israeli, siku za Uzia, mfalme wa Yuda, na siku za Yeroboamu, mwana wa Yoashi, mfalme wa Israeli, miaka miwili kabla ya tetemeko la nchi.

2  Naye alisema, Bwana atanguruma toka Sayuni, Atatoa sauti yake toka Yerusalemu; Na malisho ya wachungaji yataomboleza, Na kilele cha Karmeli kitanyauka.

3  Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Dameski, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameipura Gileadi kwa vyombo vya kupuria vya chuma;

4  lakini nitapeleka moto uingie katika nyumba ya Hazaeli, nao utayateketeza majumba ya Ben-hadadi.

5  Nami nitalivunja komeo la Dameski, na kuwakatilia mbali wenyeji wa bondeni mwa Aveni, na yeye aishikaye fimbo ya enzi katika Beth-Adini; na watu wa Shamu watakwenda hali ya kufungwa hata Kiri, asema Bwana.

6  Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Gaza, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu waliichukua katika hali ya kufungwa kabila nzima, wawatie katika mikono ya Edomu;

7  lakini nitapeleka moto juu ya ukuta wa Gaza, nao utayateketeza majumba yake.

8  Nami nitamkatilia mbali mwenyeji katika Ashdodi; na yeye aishikaye fimbo ya enzi katika Ashkeloni; nami nitaugeuza mkono wangu uwe juu ya Ekroni; na mabaki ya Wafilisti wataangamia, asema Bwana MUNGU.

9  Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Tiro, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameitia kabila nzima katika mikono ya Edomu, wala hawakulikumbuka agano la udugu;

10  lakini nitapeleka moto juu ya ukuta wa Tiro, nao utayateketeza majumba yake.

11  Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Edomu, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu alimfuatia ndugu yake kwa upanga, akatupilia mbali huruma zake zote; hasira yake ikararua-rarua daima, akaishika ghadhabu yake milele;

12  lakini nitapeleka moto juu ya Temani, nao utayateketeza majumba ya Bosra.

13  Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya wana wa Amoni, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wamewapasua wanawake wa Gileadi wenye mimba, ili wapate kuongeza mipaka yao;

14  lakini nitawasha moto katika ukuta wa Raba, nao utayateketeza majumba yake; pamoja na kupiga kelele siku ya vita, pamoja na tufani katika siku ya chamchela;

15  na mfalme wao atakwenda utumwani, yeye na wakuu wake wote pamoja, asema Bwana.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23