«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »

2 Timotheo 4

1  Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu walio hai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake;

2  lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho.

3  Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti;

4  nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo.

5  Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako.

6  Kwa maana, mimi sasa namiminwa, na wakati wa kufariki kwangu umefika.

7  Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, Imani nimeilinda;

8  baada ya hayo nimewekewa taji ya haki, ambayo Bwana, mhukumu mwenye haki, atanipa siku ile; wala si mimi tu, bali na watu wote pia waliopenda kufunuliwa kwake.

9  Jitahidi kuja kwangu upesi.

10  Maana Dema aliniacha, akiupenda ulimwengu huu wa sasa, akasafiri kwenda Thesalonike; Kreske amekwenda Galatia; Tito amekwenda Dalmatia.

11  Luka peke yake yupo hapa pamoja nami. Umtwae Marko, umlete pamoja nawe, maana anifaa kwa utumishi.

12  Lakini Tikiko nalimpeleka Efeso.

13  Lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa, ujapo ulilete, na vile vitabu, hasa vile vya ngozi.

14  Iskanda, mfua shaba, alionyesha ubaya mwingi kwangu; Bwana atamlipa sawasawa na matendo yake.

15  Nawe ujihadhari na huyo, kwa sababu aliyapinga sana maneno yetu.

16  Katika jawabu langu la kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu, bali wote waliniacha; naomba wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo.

17  Lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia nguvu, ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu, hata wasikie Mataifa yote; nami nikaokolewa katika kinywa cha simba.

18  Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina.

19  Nisalimie Priska na Akila, na wale wa nyumbani mwa Onesiforo.

20  Erasto alikaa Korintho. Trofimo nalimwacha huko Mileto, hawezi.

21  Jitahidi kuja kabla ya wakati wa baridi. Eubulo akusalimu, na Pude, na Lino, na Klaudia, na ndugu wote pia.

22  Bwana na awe pamoja na roho yako. Neema na iwe pamoja nanyi.

«  Sura ijayo   |   Chagua sura   |   Kitabu kijacho  »
“Neema ya Bwana Yesu na iwe pamoja nanyi.” — 1 Wakorintho 16:23